Loading...

Ujumbe wa Klabu ya Mbeya City kwa Simba SC

WAKATI Simba wakipiga hesabu ya kuvuna pointi zote 21 katika michezo yake iliyosalia Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kocha wa kikosi cha Mbeya City, Kinnah Phiri, amesema za kwao haziendi popote.

Mbeya City ambao tayari wamefika jijini Dar es Salaam, watakutana na Simba Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambapo Phiri ameweka wazi kuwa vijana wake wapo tayari kwa vita.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Phiri alisema kulingana na nafasi waliyokuwepo katika msimamo wa ligi, hawana budi kuhakikisha wanashinda michezo yao yote iliyobaki ili wamalize kushika nafasi za juu.

“Tunataka kumaliza ligi katika nafasi ya tano bora, hivyo ni lazima kuhakikisha tunashinda michezo yetu iliyosalia, tunajua tunakwenda kukutana na Simba lakini tutapambana mpaka dakika ya mwisho kwa lengo la kupata ushindi,” alisema.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Mbeya City wakiwa uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya, walikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Wekundu hao wa Msimbazi na sasa wanataka kulipiza kisasi.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi sasa, Mbeya City wanashika nafasi ya nane kutokana na pointi 29, Simba wao wakiongoza kwa pointi 54 baada ya kucheza michezo 23.

Source: Bingwa
Ujumbe wa Klabu ya Mbeya City kwa Simba SC Ujumbe wa Klabu ya Mbeya City kwa Simba SC Reviewed by Zero Degree on 3/02/2017 10:31:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.