Loading...

Watuhumiwa zaidi ya 100 watiwa mbaroni kwa dawa za kulevya jijini Mwanza

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi
WATUHUMIWA 142 wamekamatwa wakijihusisha na biashara ya dawa za kulevya za mazao ya shamba mkoani Mwanza katika kipindi cha Januari mosi hadi Februari 28, mwaka huu.

Hayo yamesemwa jijini hapa mwishoni mwa wiki na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Jeshi la Polisi katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Kamanda Msangi alisema dawa hizo zimekamatwa kutokana na jitihada za polisi kwa kushirikiana na wadau katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya mkoani Mwanza.

Alisema kati ya watu waliokamatwa, wanaume walikuwa 99 na wanawake 11, ambapo kulikuwa na kesi 77 za kupatikana na bangi yenye uzito wa kilo 458.

Alisema jumla ya watu 32 , wanaume 27 na wanawake 5 walikamatwa kwa kuwa na kilo 85 za mirungi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria. Kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani, alisema kulikuwa na kesi 20 za heroine, ambapo kete 66 za heroine zenye uzito wa gramu 22 na pinchi 473 zilikamatwa.

“Kulikuwa na kesi tano za watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, na jumla ya ekari 1.5 za bangi na mirungi ziliteketezwa na kesi 119 ziliripotiwa, 49 zilifikishwa mahakamani, 45 ziko katika hatua mbalimbali za kimahakama na kesi nne zimeisha kwa kupata mafanikio,” alifafanua.

Aliongeza kuwa kesi 70 zipo katika hatua mbalimbali za kiupelelezi, ambapo kati ya hizo, kesi 21 zinasubiri majibu kutoka kwa Mkemia wa Serikali, 39 zipo katika hatua ya upelelezi wa polisi na kesi 10 zimefungwa na polisi kutokana na kuwa na ushahidi dhaifu.

Alisema tatizo la dawa za kulevya ni kubwa katika mkoa wa Mwanza kwa kuwa lina maadui wa ndani na nje na linahitaji ushirikiano wa pamoja katika kulitokomeza.
Watuhumiwa zaidi ya 100 watiwa mbaroni kwa dawa za kulevya jijini Mwanza Watuhumiwa zaidi ya 100 watiwa mbaroni kwa dawa za kulevya jijini Mwanza Reviewed by Zero Degree on 3/13/2017 02:39:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.