Loading...

Sakata la mauaji askari polisi 8 mkoani Pwani laibukia bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai.
TUKIO la mauaji ya askari wanane lililotokea wiki iliyopita Kibiti, mkoani Pwani, limetinga Bungeni huku wabunge wakitaka bunge liahirishe shughuli zake kupisha jambo hilo kujadiliwa.

Wabunge jana walitaka muda wa kujadili mauaji hayo kutokana na matukio ya aina hiyo dhidi ya askari polisi kuuawa katika wilaya hiyo, kujirudia mara kwa mara.

Kutokana na hali hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilikutana jana na mawaziri wenye dhamana ili kupata taarifa rasmi kuhusiana na matukio hayo.

Ndugai alitoa kauli hiyo wakati akijibu miongozo ya wabunge waliotaka bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili suala hilo.

Alisema tayari kamati hiyo iko kazini na kupitia kikao hicho, serikali itaeleza namna ilivyojipanga kukabiliana na matukio mengine yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha hali ya usalama wa polisi, raia na mali zao.

“Niungane na waheshimiwa wote mlioonyesha kuguswa sana na suala hili la askari wetu kiwango cha kufikia wanane wakati mmoja kuuawa. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana. 

”Kwa hiyo kwa niaba ya Bunge zima hili ningependa kutoa pole na rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na kipekee kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa jambo hili kubwa ambalo limetushtua wote katika nchi yetu,” alisema. 

Alibainisha kamati hiyo inakusudia kukutana na mawaziri husika na baada ya kamati kulifahamu vyema jambo hilo ndipo bunge litaweza kujadili baada ya kamati kulifahamu kwa undani wake.

Ndugai aliwaomba wabunge kuwa watulivu na kwamba amezungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kumhakikishia kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko kazini si kwenye maeneo hayo tu bali nchi nzima.

Wabunge waliosimama kuomba mwongozo kwa Spika ni pamoja na wa Bukombe (CCM) Dotto Biteko, ambaye alitumia kanuni ya 69 kuomba kutoa hoja ya kuahirisha bunge ili kujadili suala hilo. Alisema Aprili 13, mwaka huu katika kijiji cha Makengeni wilayani humo waliuawa askari wanane na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi.

“Askari hawa walikufa wakiwa wanatekeleza majukumu ya kutulinda sisi raia na mali zetu. tukio hili si la kwanza kwa wilaya ya Kibiti. Liliwahi kutokea Februari 21, mwaka huu na watu watatu waliuawa akiwemo Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kibiti Peter Kubeza,” alisema. 

“Kama askari hawako salama kwa kiwango hiki, raia wa kawaida hali yao ikoje? Jambo hili limetokea Kibiti lakini linaweza kutokea Kongwa, linaweza kutokea Bukombe na mahali kwingine kokote kama taifa halijachukua hatua madhubuti,” aliongeza na kusisitiza: 

“Bunge lijadili ili kuondoa hofu wananchi maana kwa matukio haya yanayoendelea kutokea wana hofu kubwa juu ya usalama wao na maisha yao na mali zao juu ya matukio haya naomba tuahirishe bunge tujadili suala hili.” 

Naye, Mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdalla Masoud, aliomba suala hilo lijadiliwe na kumwomba Spika atumie busara ili suala hilo lipate nafasi.

Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, na wa Viti Maalum (CCM), Amina Mollel, pia waliunga mkono mwongozo ulioombwa na Biteko.

Hata hivyo, Spika Ndugai alitoa nafasi kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kuzungumzia suala hilo na kusema serikali inalichukulia tukio hilo kwa uzito mkubwa ili kuhakikisha wanarejesha hali ya usalama katika maeneo hayo.

Aliwatoa hofu wananchi na kusema kuwa tukio hilo limewapa chachu zaidi ya kupambana na uhalifu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira salama wao na mali zao.

Tukio la kuuawa askari hao lilitokea Alhamisi iliyopita jioni wakati polisi hao wakitoka lindo wakienda kambini.

Waliouawa ni Mrakibu Msaidizi Peter Kigugu, Koplo Francis, Konstebo Jackson, Konstebo Zacharia, Konstebo Siwale, Konstebo Maswi na Konstebo Ayoub.
Sakata la mauaji askari polisi 8 mkoani Pwani laibukia bungeni Sakata la mauaji askari polisi 8 mkoani Pwani laibukia bungeni Reviewed by Zero Degree on 4/19/2017 12:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.