Loading...

Umeisikia hii ya Mohamed Fakhi kutoweka Ghafla?

WAKATI Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikitarajiwa kutoa maamuzi ya rufaa ya Simba juu ya pointi tatu kutoka kwa Kagera Sugar baada ya kumchezesha Mohamed Fakhi akiwa na kadi tatu za njano, beki huyo ametoweka ghafla, huku simu zake zote zikiwa hazipatikani.

Inadaiwa kuwa, tangu Fakhi alipomaliza kuhojiwa na Kamati hiyo iliyokutana siku ya Jumanne kwenye Hoteli ya Protea, jijini Dar es Salaam, alionekana kwa siku mbili na baada ya hapo akatoweka.

Kwa mara ya mwisho mchezaji huyo siku ya Alhamisi mchana, alisema bado yuko jijini Dar es Salaam na alikuwa akijiandaa na safari ya kuelekea Kagera kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha timu yake kinachojiandaa na mechi za mwisho, ingawa hajafika hadi hivi sasa.

Fakhi pamoja na viongozi wa Kagera Sugar, akiwamo Mratibu Mohammed Hussein, walikuwa miongoni mwa watu walioitwa kuhojiwa na kamati hiyo, ili kutoa ushahidi kuhusiana na kadi tatu.

Wito wao ulikuja baada ya Kamati ya Saa 72, kuwapa Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, pointi tatu na mabao matatu, kwa madai kuwa Kagera Sugar ilimchezesha mchezaji huyo wakati alikuwa na kadi tatu za njano.

Hata hivyo, uongozi wa Kagera Sugar uliandika barua TFF, kuomba uamuzi huo upitiwe upya, wakidai hawajaridhika na uamuzi huo.

Tangu kuanza kwa sekeseke hilo, ambalo ndilo limekuwa habari ya mujini, Fakhi alikuwa akipatikana kirahisi, hasa kupitia kwenye mawasiliano yake ya simu, lakini tangu juzi amezima kabisa simu yake, huku viongozi wake nao wakigonga mwamba kumpata.

Simu zake zlilitafutwa, lakini zote hazikuwa zikipatikana, licha ya kwamba mchezaji huyo alikuwa jijini Dar es Salaam, ambapo alikuja kwa ajili ya sakata hilo.

Baada ya gazeti hili kufanya juhudi kubwa za kumtafuta na kushindikana, ndipo lilipoamua kupiga hodi kwa uongozi wa Kagera Sugar kujua alipo mchezaji wao huyo, ambapo Mratibu wa Wakata Miwa hao, Mohamed Hussein, naye alikiri kutokumpata kwenye simu.

“Siwezi kuzungumza mengi, ila lililopo ni kwamba tumejaribu kumpigia lakini amekuwa hapatikani, sasa hatujui alipo,” alisema kiongozi huyo juzi.

Jana pia alitafutwa, lakini simu yake haikuita na lilipomtafuta mratibu huyo, naye alikiri kwa mara nyingine kutokumpata kwenye simu yake, huku akidai kuwa walitaka kumsafirisha kwenda kujiunga na wenzake kujiandaa na michezo mingine.

Wakati hali ikiwa hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inakutana tena leo, kwa ajili ya kumalizia kupitia ushahidi wote kabla ya kuanika ukweli kuhusu ni nani hasa mmiliki halali wa pointi tatu kati ya Simba na Kagera Sugar.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Richard Sinamtwa, alisema kuwa kamati yao inakutana leo kumalizia pale walipoishia na kutoa maamuzi.

Alisema mpaka jana walikuwa hawajaipokonya Simba pointi ilizokuwa imepewa na Kamati ya Saa 72, japo kuna mambo mengi ambayo wamegundua kutoka kwa mashahidi wa kesi hiyo, hivyo wanahitaji umakini mkubwa katika kutoa maamuzi.

“Vitu tulivyokuwa tunasubiri vyote vimekamilika, hivyo (kesho) leo tutakutana kwa ajili ya kufanya majumuisho na kutoa maamuzi ya kamati,” alisema Sinamtwa.

Kuhusu shinikizo la Simba kutaka kuandamana wakidai wamekuwa hawatendewi haki na TFF, katika kesi zao nyingi, Sinamtwa alisema kuwa malalamiko ya Simba yanailenga TFF, si Kamati yake, hivyo hawezi kulizungumzia na mzungumzaji wa hilo ni Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Source: Dimba
Umeisikia hii ya Mohamed Fakhi kutoweka Ghafla? Umeisikia hii ya Mohamed Fakhi kutoweka Ghafla? Reviewed by Zero Degree on 4/23/2017 01:49:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.