Loading...

Adhabu ya kikatili ilivyokatiza maisha ya mwanafunzi wa shule ya msingi mkoani Mbeya

Mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Matwiga wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Daud Kaila (11) aliyefariki dunia kwa kufungiwa kwenye kasiki na mwalimu wake, amesema alihoji sababu za mwanaye kuwekwa ndani ya kasiki, lakini akafokewa.
Kasiki ni chumba kidogo mithili ya sefu, kilichojengwa kwa matofali na kuwekwa mlango wa nondo. Hutumika kuhifadhia nyaraka muhimu au vitu vya thamani kama fedha.

Daud na mwenzake mwenye umri wa miaka 12 (jina tunalo) aliyenusurika kifo, walifungiwa kwenye kasiki hilo, ikiwa ni adhabu kutokana na kile kinachodaiwa kuwa wanafunzi hao ni watoro na hawakufika shuleni kwa muda wa siku tano.
Mzazi wa mwanafunzi aliyefariki dunia, Jordan Kaila alisema alimpeleka mwanawe shuleni na alimweleza kuwa alikuwa anaumwa.

“Nilipomuuliza mbona huendi shuleni alinijibu anaumwa. Jana (juzi) aliniomba nimpeleke shuleni kwa kuwa pekee yake anaogopa kuchapwa na mwalimu, ndipo nikamleta hapa,” alisema mzazi huyo. 

“Mwalimu alimuuliza ni kwa nini hafiki shuleni naye akajitetea, lakini ghafla akaja mwanafunzi wa kike ofisini na kusema huyo ni mwongo. Basi mwalimu huyo akaniamuru nimchape fimbo, kweli nikamchapa fimbo tatu.” 

Alisema baada ya kumchapa alitokea mwanafunzi mwingine aliyepelekwa na mzazi wake akidaiwa kuwa ni mtoro na ndipo mwalimu huyo alipowaita wanafunzi wengine akaamuru wawaingize kwenye kasiki.

“Nilipoona wanaingizwa ndani (ya kasiki) nikamuuliza mbona unamuingiza humu? Mwalimu yule akanijibu kwa ukali, ‘wewe ondoka kazi yako imeisha na siku zote huwa tunafanya hivyo kwa wanafunzi watukutu, tutamtoa muda si mrefu’. Basi mimi nikamuogopa mwalimu yule ikanibidi niondoke,” alisema. 

Mzazi huyo alisema baadaye mchana akiwa katika shughuli zake aliulizwa na jirani yake sababu za kuwepo nyumbani wakati mwanaye hali yake si nzuri na amepelekwa zahanati.

Alisema alikwenda shuleni, lakini hakupewa ushirikiano na baadaye ilibainika kuwa mtoto wake amefariki dunia na mwili wake ulikuwa kituo cha afya cha Mtanila.

Polisi wazungumza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari alisema kuwa chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo ni kukosa hewa.

Alisema baada ya muda mfupi kupita na kasiki kufunguliwa, Kaila, aliyekuwa darasa la kwanza, hakuwa akipumua vizuri, hivyo walipelekwa zahanati ya kijiji cha Matwinga kwa ajili ya matibabu lakini ilibainika Kaila alikuwa ameshafariki dunia.

Kamanda Kidavashari alisema polisi wanaendelea kumsaka mtuhumiwa ambaye ni mwalimu mkuu na anadaiwa kutoweka baada ya kusikia kifo cha mwanafunzi huyo.

Alisema mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu zake usiku wa kuamkia jana.

Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya, ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Rehema Madusa ilisafiri kutoka Chunya mjini, takriban kilomita 140 kwenda kijijini hapo.

Madusa alitoa amri kwa vyombo vya dola kumtafuta mwalimu huyo popote alipo na kuwataka wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano.

Mwanafunzi aliyenusurika: 

Mwanafunzi aliyenusurika ambaye anasoma darasa la nne shuleni hapo, alisema hakufika shuleni kwa siku kadhaa kwa kuwa alikuwa akiumwa kichwa na tumbo na alipoulizwa na baba yake mzazi alimjibu hawezi kwenda kwa kuwa ni mgonjwa.

Alisema baba yake alimununulia dawa na alipopata nafuu alimuomba mzazi wake amsindikize shuleni juzi ili akamtetee asiadhibiwe.

“Nililetwa na baba na mwenzangu aliletwa na mzazi wake. Tulipofika mwalimu aliita wanafunzi kama wanne akawaambia watuingize humu ndani (kwenye kasiki). Mimi nilikuwa chini na mwenzangu alikuwa juu,” alisema. 

“Walipotuingiza walifunga kufuli, tulipiga kelele lakini hawakutufungulia hadi tukaamua kunyamaza. Baadaye niliona mwenzangu ananidondoshea mate. 

“Tulikaa kuanzia kama saa 2:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi. Sikujua nimetoka vipi humu ndani, nilijikuta nipo nje nikihema kwa shida wakati mwenzangu akiwa anatokwa na mate kwa wingi mdomoni.” 

Mwanafunzi huyo alisema aliwahi kushuhudia mwalimu huyo akiwapa adhabu ya aina hiyo wanafunzi wengine.

Mwalimu mkuu msaidizi:

Mwalimu mkuu msaidizi wa shuleni hiyo, John Samira alisema wakati tukio hilo likitokea, alikuwa akisahihisha mitihani ya wanafunzi wa darasa la nne.

Alisema alipigiwa simu na walimu wenzake akijulishwa kuna wanafunzi wamepatwa na tatizo hivyo afike shuleni.

Samira alisema alipofika alikuta mwanafunzi mmoja akiwa amekalishwa nje ya ofisi ya mwalimu mkuu akionekana kuwa dhaifu na alipouliza kilichotokea aliambiwa walikuwa wamefungiwa ndani ya kasiki.

“Nikaambiwa mwanafunzi mwingine wamempeleka zahanati, hali yake si nzuri. Hapo nikauliza ina maana tatizo limekuwaje hadi kufikia hatua hii. Kwa kweli sikupata jibu kutoka kwa wenzangu kwa kuwa mwalimu mkuu aliyehusika na tukio hili hakuwapo na hata nilipojaribu kumpigia simu hakupatikana,” alisema. 

Alisema aliamua kwenda kwenye zahanati hiyo na hapo alikuta hali ya mwanafunzi huyo ikiwa mbaya na wauguzi walimwambia inabidi apelekwe kituo cha afya cha Mtanila kwa matibabu zaidi, lakini alipofika huko walielezwa alikuwa ameshafariki dunia.

Daktari azuiwa kuzungumza

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Madusa aliyefika eneo la tukio na baadaye kwenda kituo cha afya saa 2:00 usiku, alimuagiza daktari aliyeongozana naye kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo cha mtoto huyo.

Baada ya uchunguzi kufanyika, Madusa alimzuia daktari huyo kutoa taarifa kwa waandishi wa habari akisema uchunguzi bado unaendelea.
Adhabu ya kikatili ilivyokatiza maisha ya mwanafunzi wa shule ya msingi mkoani Mbeya Adhabu ya kikatili ilivyokatiza maisha ya mwanafunzi wa shule ya msingi mkoani Mbeya Reviewed by Zero Degree on 5/11/2017 12:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.