Loading...

Makumbusho ya kuhifadhia radi asili kujengwa mkoani Rukwa

JUMUIYA ya Maendeleo Mkoa wa Rukwa (JUMARU), imeitembelea nchi jirani ya Zambia katika mji wa Mbala kwa lengo la kwenda kujionea na kujifunza uhifadhi wa mambo ya asili na utamaduni.

Ujumbe huo uliongozwa na Katibu mkuu wa JUMARU taifa, Anatory Sikulumbwe, ulifadhiliwa na serikali kwa msaada wa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk. Khalfan Haule, aliyewasiliana na Serikali ya Zambia kupitia Mkuu wa Wilaya ya Mbala, Kedrick Sikombe.

Sikulumbwe alisema lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujifunza namna majirani zao wanavyoweza kukusanya, kuanzisha na kuhifadhi vitu vya jadi na asili ili waanzishe makumbusho yatakayokuwa kielekezo na historia kwa kizazi cha sasa na baadaye.

Alisema wakiwa Zambia walijifunza mambo mbalimbali ambayo mengine yalichukuliwa kutoka nchini Tanzania kutoka kwa kabila la Walungu na Wamabwe na kuhifadhiwa nchini Zambia katika makumbusho yao na kunufaika nayo.

Alisema jumuiya hiyo inatarajia kuanzisha makumbusho katika mji wa Milanzi, mjini Sumbawanga itakayohifadhi na kutunza sehemu ya tiba za jadi na tafiti mbalimbali zitakuwa zikifanyika kuhusu mambo ya asili ya Mkoa wa Rukwa.

Sikulumbwe alisema wameshapata eneo la kujenga makumbusho hayo na Shilingi bilioni nane ambazo zitatumika katika ujenzi wa makumbusho hayo ambayo yatakuwa makubwa kutokana na vitu vitakavyo hifadhiwa na shughuli zitakazofanyika ili watu waweze kwenda kutembelea kujifunza historia na kupata tiba za jadi.

Alisema taratibu zote zimekamilika kwa mujibu wa sheria za nchi ndiyo maana serikali ipo pamoja nao na uzinduzi wa ujenzi wa makumbusho hayo utazinduliwa rasmi Mei 28, mwaka huu.

Alisema makumbusho hayo yatakuwa ni fursa muhimu kwa wananchi sio tu wa mkoa wa Rukwa, bali nchi nzima na kwa shughuli za tiba za jadi na sehemu muhimu ya kitalii ndani na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa mambo ya jadi na utamaduni wa kituo hicho, Gerrmano Wanchelele, alisema watajitahidi kutoa na kutafuta vitu vya jadi ili vihifadhiwe ikiwamo radi ya asili ambayo zimekuwa ikitumika kama silaha ya kulipiza kisasi.


Credits: Nipashe
Makumbusho ya kuhifadhia radi asili kujengwa mkoani Rukwa Makumbusho ya kuhifadhia radi asili kujengwa mkoani Rukwa Reviewed by Zero Degree on 5/21/2017 09:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.