Loading...

Mtoto afariki dunia baada ya kula mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu

Mtoto wa miaka mitatu amefariki dunia, huku wanafamilia wengine 10 wakinusurika baada ya kula mihogo ya kuchemsha inayosadikiwa kuwa na sumu.

Tukio hilo lilitokea Mei 19 eneo la Mbondole Manispaa ya Ilala.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbondole, Thomas Nyanduli alisema alipewa taarifa kuwa familia ya Chacha Fyefye yenye watu 11 ilipatiwa matibabu katika zahanati ya Kivule baada ya kula mihogo hiyo.

Nyanduli alisema wengine walihamishiwa Hospitali ya Rufaa Amana ambako baada ya matibabu waliruhusiwa kutokana na afya zao kuimarika.



“Chacha ana watoto tisa pamoja naye na mkewe jumla wapo 11, nilipewa taarifa kuwa siku ya tukio mkewe baada ya kumaliza kuuza mboga eneo la Viwege alinunua mihogo na kwenda nayo nyumbani bila kujua ilikuwa na kitu gani aliipika kwa ajili ya chai. 


“Hatuwezi kuthibitisha kama ilikuwa ni sumu ya namna gani, lakini mtoto mmoja amepoteza maisha baada ya kula mihogo hiyo na wengine wameruhusiwa kurejea nyumbani na wanaendelea vizuri,” alisema Nyanduli. 

Dereva wa bodaboda, Daud Mseti alisema akiwa kituoni alifuatwa na kutakiwa kwenda nyumbani kwa Chacha kwa ajili ya kuwachukua wagonjwa awapeleke hospitali.

Alisema walipofika nyumbani kwa Chacha, aliwakuta watoto watatu wakiwa wamelazwa chini ambao aliwapakia kwenye pikipiki na kuwapeleka zahanati kwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alithibitisha kutokea tukio hilo akisema wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo. “Juzi nilipata taarifa kuhusu mtoto wa miaka mitatu kufariki dunia akidaiwa kula mihogo yenye sumu na watu wawili ambao mama na mtoto walilazwa katika Hospitali ya Amana,” alisema Hamduni.
Mtoto afariki dunia baada ya kula mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu Mtoto afariki dunia baada ya kula mihogo inayosadikiwa kuwa na sumu Reviewed by Zero Degree on 5/22/2017 08:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.