Loading...

Simba yasusia zawadi za Ligi Kuu ya Vodacom [VPL]

Klabu ya Simba imegoma kuchukua zawadi ya mshindi wa pili mara baada ya mchezo wake wa mwisho wa ligi kuu Tanzania bara dhidi ya Mwadui FC.

Licha ya ushindi wa Simba wa magoli 2-1 na kufikisha alama 68 sawa na Yanga ambayo imepoteza mchezo wake wa mwisho kwa kufungwa 1-0 na Mbao FC, bado Simba imejikuta ikimaliza katika nafasi ya pili kutokana na tofauti ya wastani wa magoli.

Baada ya mchezo wa Simba vs Mwadui kumalizika kwenye uwabja wa taifa, MC alitangaza kwamba timu ya Simba itapewa zawadi kulingana na nafasi waliyomaliza (ya pili) huku Yanga wakiwa wametwaa ubingwa wa VPL 2016/17.

Jambo la kustaajabisha ni pale viongozi na wachezaji kuonekana kutojali zawadi hiyo, walielekea vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya mchezo.

Walisubiriwa kwa dakika kadhaa lakini hawakutokea, walipoulizwa baadhi ya viongozi walijibu kwamba wachezaji wanabadili jezi walizochezea na kuvaa nguo maalum kwa ajili ya kwenda kupokea zawadi hizo.

Kadiri muda ulivyozidi kuyoyoma bado Simba waliendelea kusalia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na mara kadhaa wachezaji na viongozi walitoka na kurudi tena vyumbani.

Waandishi wa habari waliokuwepo uwanjani kwa ajili ya kushuhudia tukio hilo walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine na kuwaacha wachezaji wa Simba wakiwa bado hawajatoka ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo.

Imebainika kwamba Simba walikua wameandaliwa medali kama zawadi ya mshindi wa pili.

Makamu mwenyekiti wa Simba Geoffrey Nyange Kaburu amesema hawawezi kuchukua zawadi ya mshindi wa pili kwa sababu wanasubiri malalamiko yao yafanyiwe kazi na FIFA ndipo watajua kama nafasi yao ni ya pili au vinginevyo.

Inaelezwa kwamba, endapo Simba wangekubali kuvaa medali za nafasi ya pili basi wangelazimika kusaini kitabu maalum ili kuweka kumbukumbu kuhusu nafasi waliyomaliza katika ligi kwa msimu husika.

Simba wamemaliza ligi wakiwa nyuma ya Yanga kwa tofauti ya wastani wa magoli 10, Yanga wanawastani wa magoli 43 wakati Simba wao wana wastani wa magoli 33 huku timu zote zikiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 30.
Simba yasusia zawadi za Ligi Kuu ya Vodacom [VPL] Simba yasusia zawadi za Ligi Kuu ya Vodacom [VPL] Reviewed by Zero Degree on 5/20/2017 11:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.