Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 02


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia…………..Sauti za mlio wa mtarimbo juu ya mwamba ndiyo iliyokuwa imetawala huku mwangwi nao ukienda sambamba na mapigo hayo ukimaanisha kuwa mtarimbo haujakosea vijia na muda si mrefu lulu itakuwa hadharani huku mtarimbo ukisafishwa kwa vimiminika vya maji kutoka kwenye matabaka ya miamba ya mahaba iliyozungukwa kwa vinyasi chupuki vilivyotulia mithili ya zile zinazosubiri kumwagiliwa na mvua za kwanza za vuli.


Endelea nayo mwenyewe: Nikiwa ni mtoto wa saba kati ya watoto kumi na tatu wa kiume wa mzee Sikitiko, nilikuwa mtoto mwenye nidhamu na heshima ya hali ya juu jambo ambalo lilinifanya nipendwe na wazazi wangu, jamii yote na hata walimu wangu kwa ujumla. Kupendwa kwangu hakukunifanya niyabwetekee yale maisha mazuri ya pale nyumbani bali iliniongezea chachu ya kuyakabili na kuyaandaa maisha yangu ya kesho. Katika vitu ambavyo sikuvifanyia ajizi ni pamoja na suala zima la kuishikilia imani ya mafundisho kwa mujibu wa dini yangu. Nilikuwa ni miongoni mwa watoto waliyofuata imani na mafundisho ya dini kwa kuyashika kwa kiwango cha juu. Miongoni mwa misemo iliyonihamasihsa au iliyonipa changamoto ya kupambana na maisha ni ile isemayo ………”Mkamateni elimu msimwache aende zake…..” na ule usemao, “Nitawafanya kuwa vichwa wala si mikia”.

********

Nilipambana na harakati za maisha kwa kujishughulisha na kazi za shamba bila hata chembe ya uvivu huku masomo ya darasani nikiyahusudu bila ajizi. Nilipendwa na makundi yote ya wanafunzi wa eneo letu na hasa pale nilipoongoza kwenye mitihani ya muungano kwa shule nane nami kuwa kinara kwa ufaulu wa juu zaidi. Kwa matokeo hayo kila mwanafunzi alipenda aunge urafiki na mimi au anifahamu kwa sura. Binafsi nilijisifia sana huku nikimrudishia mola wangu sifa na utukufu. 

Vijana wengi walikuwa wakimiminika nyumbani kwetu kwa minajili ya kubadilidshana nao mawazo ya kielimu na ya kijamii kwa ujumla. Upendo wangu haukuishia hapo kwani ulivuka mipaka na kuelekea vijiji jirani kwa kasi ya ajabu. Hii ilitokana na uwezo wangu wa darasani na ule wa kushiriki makambi ya vijana yaendeshwayo kikanisa kwa lengo la kuwakutanisha vijana kutoka sehemu tofauti kwa kufanya maonesho mbalimbali ya sanaa za maonesho na kuyajadili matatizo ya vijana kwa ujumla. Moja ya mada niliyowahi kuiwasilisha kwa vijana wenzangu iliyonifanya nifahamike zaidi ni ile isemayo, “Kijana ujitunze kwa kuuheshimu ujana wako”. Niliyadadavua mambo yanayoiathiri jamii na hasa vijana kutoyafikia malengo au ndoto za maisha yao. Machache ya mambo hayo ni kama vile, ukosefu wa elimu ya malezi ya ujana, ujasiriamali, mahusiano kabla ya ndoa, jicho la serikali kwa vijana na vijana na mitazamo yao. Hizo ni baadhi ya mada zilizonifanya nifahamike kuliko ninavyojifahamu. Nyumbani kwetu hapakuwahi kukosekana kwa wageni kila uchao na wengi walikuwa wakinihusu mimi, huku wengi wakiwa ni wale wa kike ingiwa na wakiume hawakukosekana. Ikafikia wakati nikiwa nataka nisiwe karibu na jamii kwani ugeni huo niliuhesabu kama usumbufu kwani nilikuwa nikabiliwa na hitimisho la mitihani yangu ya kumaliza elimu ya msingi.

********

Nikiwa katika maandalizi ya mitihani yangu ya mwisho nilibahatika kukabidhiwa mwanafunzi mwenzangu wa kike ambaye naye ni miongoni mwa wanafunzi walioko mbioni kuhitimu elimu ya darasa la saba, ili tujisomee pamoja. Wiki ya kwanza katika masomo yetu ilikwenda vema kabisa huku kila mmoja akiuwazia mtihani tu. Kila siku nilikuwa sisahau kuyapitia maneno ya Mungu katika kitabu cha Imani yangu, jambo ambalo wenzangu walianza kunitabiria utabiri wa kuja kuwa kiongozi mkuu wa dini. Katika msafara wowote wa mamba mara nyingi, kenge huwa hawakosekani na safari ya nzige hata panzi huitwa nzige na ndivyo ilivyokuwa katika kundi la wanafunzi wa darasa letu. Kulikuwa na wale wenzangu na mimi wenye majina ya Sitakishule, wanaotumia mihadarati, waliojiingiza kwenye mambo ya ngono na wengine uchezaji wa kamali kwenye ‘magheto’. Miongoni mwa wanafunzi ambao ilisemekana kuwa ni mafundi sanifu katika biashara ya ufusika ni huyu waliyeniletea nisome naye. Msichana huyu akiitwa mwadawa alikuwa ni dawa kweli kweli ya kuwapoza vijana wenzake maganzi na hata watu wa zima wenye muono hafifu wa maadili wanaoamini kuwa kwenye mapenzi hakuna mtoto ila mtoto ni yule uliyemzaa tu.

********

Mwanafunzi huyu alianza kunipotezea muda wa kusoma kwani kila wakati yeye alikuwa akinisimulia hadithi za ngono kutoka kwenye mitandao mbalimbali ukiwemo ule wa Facebook ulionitoa ushamba nilipotoa tafrisi sisisi, yaani uso wa kitabu. Niliendelea kumzoea na vihadithi vyake hivyo ambavyo muda mwingine viliniamsha hisia Fulani za kimapenzi za kutaka kuijaribisha bahati yangu kwa Mwadawa ya kutaka dawa lakini nafsi yangu ikiniambia kwa maneno ya moyoni kwamba, “Muda wako wa mapenzi bado haujafika hivyo acha utamu na vitamu vikupite”. Niliyaheshimu mawazo ya moyo wangu kwa kumchukulia Mwadawa kama miongoni mwa dada zangu na kikubwa nilimuhimiza akikamate kitabu sawasawa ili aje awe wakili au mwanasheria msomi atakayeweza kuja kuwakomboa wanawake wanyonge wanaonyanyaswa na mifumo dume isiyorafiki kwa wanawake pia aje kuwa mtaalamu wa sheria za mikataba ya kimataifa inayosababisha nchi yetu kuingia mikataba isiyo na tija kama ile ya madini hapa Tanzania. 

********

Mwadawa alianza kubadilika taratibu kitabia mpaka wanajamii walishtushwa na mabadiliko ya haraka ya msichana huyo aliyekuwa akihusudu ngono kama ubweche kwa watoto. Kubadilika kwa Mwadawa kulimfanya atabiliwe kwa mambo mengi sana likiwemo la kufika mbali sana kielimu. Mitihani ilfanyika na matokeo yalipotoka jina langu la David Sikitiko lilikuwa la kwanza juu kabisa na la Mwadawa kusomeka kwenye namba kumi na moja. Familia zetu na za wanafunzi wengine waliochaguliwa zilikuwa na furaha isiyo ya kifani.

====>>Itaendelea Ijumaa...

Usiikose SEHEMU YA 03>>> ya Riwaya hii ifikapo ijumaa ya wiki inayofuata, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 02 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 02 Reviewed by Zero Degree on 6/05/2017 05:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.