Loading...

Halima Mdee, Ester Bulaya wamesimamishwa kuhudhuria Bunge hadi mwaka 2018


Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya wote wa CHADEMA wameadhibiwa kwa kusimamishwa na Bunge kuhudhuria vikao vyote vilivyosalia vya mkutano wa 7 wa Bunge la Bajeti linaloendelea hivi sasa mjini Dodomaa, pia hawatohudhuria mkutano wa 8 na wa 9 kwa utovu wa nidhamu.

Aidha Bunge limeamua kuwa, wabunge hao watarudi kuhudhuria vikao kuanzia kwenye Bunge la Bajeti mwaka ujao (2018/2019). Hukumu hiyo imeungwa mkono na wabunge wengi waliopitisha azimio hilo. Mapema leo, Jumatatu Kamati ya Maadili ilisema Bulaya na Mdee wamemaliza adhabu za kawaida zilizopo kwenye kanuni za bunge.

Hata hivyo, Bunge liliendelea kujadili makosa ya wabunge hao wa Bunda na Kawe. Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika aliliomba Bunge kujadili adhabu inayostahili kulingana na makosa yao.

Kanuni inasema, mbunge anayefanya kosa la kwanza anaweza akazuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 10 na atayakosea kwa mara ya pili anaweza kuzuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 20.

Tukio hilo limeibuka kufuatia vurugu zilizoibuka Ijumaa iliyopita baada ya Mbunge wa Mvumi, Livingstone Lusinde kudai kwamba wapinzani bungeni humo wanatetea wezi wa mchanga wa dhahabu, hali iliyosababisha Mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuibuka na kubishana. Mbunge mwingine ambaye hakujulikana jina lake aliwasha maiki na kumuita Mnyika mwizi, Mnyika alikitaka kiti cha Spika kimuamuru mbunge huyo kufuta kauli yake lakini spika alisema hakumsikia aliyesema maneno hayo.

Baada ya mabishano kati ya Spika na Mnyika, spika aliamuru Mnyika atolewe nje na polisi wa Bunge, hali iliyosababisha Halima Mdee na Ester Bulaya, waiingilie kati kuwazuia askari hao kumtoa nje. Jambo hilo lilisababisha tafrani licha ya Mnyika kutolewa nje huku wabunge wa upinzani wakitoka nje.

Spika alitangaza kumsimamisha Mnyika asihudhurie vikao vya bunge kwa wiki moja huku akisema Ester Bulaya na Halima Mdee wataandikiwa barua ili wakahojiwe na Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge ambapo leo wameadhibiwa wasihudhurie vikao vya bunge kama ilivyoelezwa hapo mwanzo.
Halima Mdee, Ester Bulaya wamesimamishwa kuhudhuria Bunge hadi mwaka 2018 Halima Mdee, Ester Bulaya wamesimamishwa kuhudhuria Bunge hadi mwaka 2018 Reviewed by Zero Degree on 6/05/2017 06:30:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.