Loading...

Utata waibuka mazishi ya Philemon Ndesamburo

Hali ya sintofahamu jana ilikuwa imetanda msiba wa mwanasiasa mkongwe nchini, Philemon Ndesamburo baada ya Serikali ya mkoa kutaka shughuli ya kuaga mwili wake ihamishwe kutoka uwanja maarufu wa Mashujaa.

Hali hiyo iliibuka baada ya uongozi wa Chadema wa Wilaya ya Moshi kupokea barua yenye kumbukumbu namba MMC/A.20/1/VOL.XV11/107, inayoeleza kuwa siku ya Jumatatu kuna taasisi za umma kama mahakama itakuwa ikiendelea na shughuli zake.

Barua hiyo ya Juni 2 iliyotumwa kwa mwenyekiti wa Chadema wa Moshi, African Mlay inasema shughuli ya kuaga mwili wa Ndesamburo aliyefariki dunia ghafla mapema wiki hii, ifanyike Uwanja wa Majengo.

“Uwanja wa Majengo ni mkubwa zaidi na ni jirani na nyumbani kwa marehemu. Una wigo, una milango ya kuingia na kutoka na una uwezo kuruhusu kuegesha magari mengi ndani,” inasema taarifa hiyo. 

Lakini, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, pamoja na kuamua kutoitia najisi shughuli ya kumuaga mwanasiasa huyo, sababu zilizotolewa hazina maana.

“Kuhama uwanja si jambo lililotushangaza, ila sababu za kuhamishwa uwanja ndio jambo ambalo limetushangaza. Niseme hizi sababu ni za kitoto na ni sababu za kijinga,” alisema Mbowe. 

Mbowe alisema uwanja wa Mashujaa umekuwa ukitumika kwa mikutano ya kampeni na matamasha miaka mingi na mahakama ilikuwa ikiendelea na shughuli zake na hapajawahi kuwa na tatizo.

Alisema hata Uwanja wa Majengo uko karibu na Shule ya Sekondari Majengo, Kituo cha Afya cha Majengo na makazi ya wananchi.

“Je, na huko nako hatutawasumbua watu?” alihoji. 

“Tumekaa na kutafakari kwa kina kama chama na kwa kushauriana na familia. Tunalichukua hili kama hujuma za kijinga za kisiasa. Zinajenga chuki na kuanza kututenga Watanzania. 

“Sisi tumeona hakuna sababu ya kutia najisi zoezi zima na mchakato mzima wa kumuaga Ndesamburo. kwa hiyo tumekubali kufanyia hapo Majengo. Tutafanya maandalizi usiku na mchana." 

Mbowe pia alikumbushia mazishi ya mwenyekiti wa Chadema wa Geita, Alphonce Mawazo ambayo Serikali pia ilitia mkono.

“Matumizi ya polisi kwa waommbolezaji si jambo la kwanza kutokea kwa Chadema. Wakati tukimuaga Alfonce Mawazo kule Mwanza iliingilia hivi hivi,” alisema. 

“Hawa wa Kilimanjaro hawajatunyima kumuaga, bali wametunyima uwanja tulioupenda kuutumia kumuaga mzee wetu Ndesamburo. Hatutaki kuingia kwenye mivutano ya kwenda mahakamani. 

“Hata wangesema tukafanyie shambani tungeenda na tutamuaga mzee wetu kwa heshima kubwa. Watapata aibu kubwa wale wanaotaka kuona msiba wa baba yetu unakosa watu na kukosa msisimko.” 

Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa Mbowe, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na mbunge wa Kibamba, John Mnyika walionekana wakikagua Uwanja wa Majengo.

Taharuki

Hali ilikuwa ni ya taharuki katika Uwanja wa Mashujaa ambako kulitokea mabishano makali kati ya wabunge wa Chadema na Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Moshi (OCD), Pancras Mdimi.

Wabunge hao, Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Selasini (Rombo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini) walibishana na OCD huyo ambaye alitishia kutumia nguvu kama akipewa amri.

OCD huyo pamoja na maofisa wa polisi waliovalia sare na askari kanzu walikwenda uwanjani hapo saa 7:00 mchana na kutaka shughuli zote za maandalizi zisimame.

Wakati amri hiyo ikitolewa, tayari wanachama na viongozi wa Chadema walikuwa wakiendelea kusafisha eneo hilo na kuanza kusimika vyuma kwa ajili ya maturubai na kupanga viti.

Selasini alimsihi OCD huyo avute subira na asitumie nguvu kuwaondoa kwa kuwa mwenyekiti wao alikuwa anawasiliana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Tunasubiri maelekezo. Hii hali mnayoanza kuijenga hapa kwa kweli si utamaduni wa wananchi wa Moshi,” alisema. 

Selasini alisema hata kama Waziri Mkuu atakubaliana na uamuzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wa kutaka shughuli hiyo ifanyikie Uwanja wa Majengo, Chadema haitakubali.

“Nataka niwaambie (polisi) kama hatutaruhusiwa kumuaga mzee wetu hapa, hata huko Majengo hatutaenda. Tutaenda kumuagia nyumbani kwake na hatutahitaji ulinzi wenu,” alisisitiza. 

Kwa upande wake, Lema alisema kama umma ukiamua kumuagia Ndesamburo uwanjani hapo, hakuna mtu anayeweza kuzuia na kuonya polisi na Serikali wasigeuze Moshi kama Arusha.

“Hiki mnachokifanya tunakilaani kwa nguvu zote. Shughuli mbalimbali za kiserikali na nyingine zimefanyika hapa na hakujawahi kuwa na hoja ya ukaribu na mahakama au shule,” alisema. 

Hata hivyo, OCD huyo alisema yeye anatekeleza maagizo.

Mrisho Gambo atajwa

Kabla ya kupatikana kwa barua ya kuhamisha shughuli hiyo, kulisambaa taarifa mitandaoni zikimtuhumu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kutia mkono katika uamuzi huo.

Hata hivyo, Gambo, ambaye anakaimu ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro, amesema hajazuia mwili wa Ndesamburo kuagwa uwanjani hapo na kwamba suala hilo ni la Manispaa ya Moshi.

Gambo alisema uongozi wa Moshi ndiyo umeshauri kubadilishwa uwanja kutokana na sababu mbalimbali zikiwepo za kiusalama na ukubwa wa uwanja.

“Lakini kama kuna malalamiko juu ya mabadiliko ya uwanja, ni vyema wanaolalamika wakawasiliana na mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi ili kupata muafaka kuliko kulifanya jambo hili kuwa la kisiasa,” alisema. 

Gambo alisema kwa taarifa ambazo amepata Uwanja wa Majengo ungefaa kwa kuwa ni mkubwa, una njia za kutosha za kuingia na kutoka na kiusalama ni mzuri zaidi.

Alisema hakuna kiongozi wa Serikali ambaye anaweza kuzuia kuagwa mwili wa Ndesamburo kwa kuwa ana heshima yake na ni vyema kushirikiana kumuhifadhi.

“Lengo letu ni kumhifadhi Mzee Ndesamburo hivyo tushirikiane, lakini kwa kuwa maombi ya uwanja walipeleka kwa Mkurugenzi na yeye ndiye ameshauri kutumika uwanja mwingine, ni vyema wakarudi kushauriana,” alisema.

Kikwete awaza kuhudhuria:

Wakati hali ikiendelea hivyo, Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete anatafakari uwezekano wa kushiriki shughuli ya kuaga mwili wa mwanasiasa huyo.

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini aliiambia Mwananchi jana kuwa alipigiwa simu na Kikwete juzi, akisema angetamani kushiriki kuaga mwili wa Ndesamburo kesho kwenye Uwanja wa Mashujaa.

Selasini alisema Kikwete alimueleza anatarajia kwenda ziarani Ethiopia na hivyo anaangalia uwezekano wa kufanikisha yote mawili.

“Rais mstaafu alisema ametamani sana kushiriki katika mazishi, lakini ana ziara isipokuwa anatafuta namna ambayo ataweza kufanya ili aweze kushiriki,” alisema Selasini. 

“(Kikwete) Alisema aidha anaweza kuja Jumatatu (kesho) ili Jumanne aendelee na safari yake.” 

Ndesamburo (82) ambaye alikuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo kuanzia mwaka 2000, alifariki dunia ghafla Jumatano.

Alikuwa akisaini hundi ya rambirambi kwa ajili ya familia za watoto wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent waliofariki dunia katika ajali ya gari kabla ya kuishiwa nguvu na kuwahishwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, ambako baadaye alifariki dunia.

Alikuwa akisaini hundi hiyo katika ofisi yake iliyoko majengo ya Hoteli ya Keys anayoimiliki.

Viongozi wamiminika Moshi

Wakati huohuo, viongozi mbalimbali jana waliendelea kufika nyumbani kwa Ndesamburo kwa ajili ya kutoa pole kwa wafiwa na miongoni mwa waliofika ni Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Dk Tulia alisema marehemu alifanya kazi nzuri kwa Taifa na wakati vyama vingi vilipoingia nchini yeye alipata nafasi ya kuwalea viongozi kwa upande huo.

Naibu Spika alisema maisha yake kabla ya vyama vingi alikuwa akilea watoto wengi nchini.

“Kwetu alikuwa ni kiongozi, wengine alikuwa anaonyesha njia na alikuwa mtu ambaye asingeweza kukusifia kwa jambo ambalo umekosea. Lazima atakwambia kama umekosea. Alikuwa anafanya hivyo ili ujue njia nzuri ya kuendelea mbele,” alisema Dk Tulia. 

Dk Tulia alisema wanahuzunika kwa msiba, lakini wanafarijika kwa yale aliyokuwa amewaachia na kuahidi kuyaendeleza na kuyaenzi mafundisho yake mema ya upendo na amani.

“Hajatuacha tukiwa wakiwa ametuacha na mafundisho, watoto wake watapata nafasi ya kujiangalia kwenye mioyo yao na yale aliyowafanyia. Hata sisi watoto wa nje tunayo mengi aliyotufanyia,” alisema. 

Alisema marehemu aliwalea vizuri na ndio maana wanaweza kusimama na kusema mazuri yake akitaka wengine waige mfano ili watakaobaki nao waweze kusimulia mazuri yao.

Viongozi wengine waliofika msibani jana ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecki Sadick.

Wengine ni mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, mbunge wa Kigamboni (CCM), Faustine Ndugulile, viongozi mbalimbali wa dini, wa kisiasa na wananchi mbalimbali.

Source: Mwananchi
Utata waibuka mazishi ya Philemon Ndesamburo Utata waibuka mazishi ya Philemon Ndesamburo Reviewed by Zero Degree on 6/04/2017 10:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.