Loading...

Watu 3 wamehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kukutwa na mguu wa Twiga


MAHAKAMA ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, imewahukumu kifungo cha jumla ya miaka 60 jela washtakiwa watatu waliotiwa hatiani kwa kukutwa na mguu wa twiga kinyume cha sheria za wanyama pori.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Teotimus Swai, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.

Awali, mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Jamila Miraji, alisema mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walikamatwa Oktoba 11, mwaka jana saa 5:30 wakiwa na mguu wa twiga kinyume cha sheria za wanyama pori.

Aliieleza mahakama hiyo kwamba washtakiwa walikamatwa na askari wa Tanapa waliokuwa katika doria ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Katavi, ambako waliwakuta na mguu huo wa twiga.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu Swai alisema ushahidi uliotolewa mahakamani na upande mashtaka umewatia hatiani watuhumiwa hao.

Kabla ya hukumu hiyo, hakimu Swai alitoa nafasi ya kujitetea kwa watuhumiwa, ambao waliiomba mahakama isitoe adhabu kali kwao kwa kuwa ni wategemezi, maombi ambayo yalitupiliwa mbali.

Waliohukumiwa kwenda jela ni Juma Kinanda (66), Saidi Shabani (42) wote wakazi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora na Rashidi Miraji (64) mkazi wa Inyonga wilayani Mlele.
Watu 3 wamehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kukutwa na mguu wa Twiga Watu 3 wamehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kukutwa na mguu wa Twiga Reviewed by Zero Degree on 6/07/2017 10:09:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.