Loading...

Dawasco kuunganisha maji kieletroniki ndani ya siku 7


Shirika la MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limezindua mfumo mpya wa mawasiliano ambao unalenga kumrahisishia mteja kupata na kutoa taarifa zinazohusu huduma hiyo kwa haraka.

Huduma hiyo itapatikana kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani ambapo mteja mpya ataweza kuunganishiwa maji ndani ya siku saba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Teknolojia (TEHAMA) wa DAWASCO, Kiula Kingu amesema lengo kuu la mfumo huo ni kumuweka mteja karibu kihuduma.

Alisema kuwa ili mteja kunufaika na mfumo huo anatakiwa kuhakikisha ana simu ya mkononi ya “Smartphone” ambayo itamwezesha kupakua mfumo huo na kujisajili kwa kuingiza akaunti namba yake ya DAWASCO.

“Wateja wetu watajiunga kwenye mfumo huu kwa kingiza namba ya akaunti yake ya dawasco ambapo baada ya kufuata hatua zote atatumiwa neno la siri ambalo litamwezesha kuingia na kupata taarifa husika,”alisema Kingu. 

Aliongeza kuwa Dawasco imeona ipo haja ya kujiboresha na kwenda na teknolojia kwa kumuwezesha mteja kupata taarifa kupitia simu ya mkononi muda wowote.

Naye, Meneja Uhusiano wa DAWASCO, Everlasting Lyaro, amewataka wananchi wa Dar es Salaam na Pwani kupakua mfumo huu kwani ni rahisi kuutumia na hauna gharama zozote.

Alisema kuwa mfumo huo utamrahisishia mteja kupata taarifa muhimu zinazohusu huduma ya maji zikiwamo ankara ya mwezi, taarifa za lini mteja alifungiwa huduma ya maji, muda ambao alifanya malipo, lini mita yake ya maji ilisomwa na taarifa nyingine nyingi.

“Nawasihi wateja wetu na wananchi wote kupakua mfumo huu mpya katika simu zenu za mkononi ili kuweza kufurahia huduma zetu, hakuna gharama zozote ambazo utatozwa. "

Kupitia mfumo huu utaweza kupata taarifa zote muhimu za huduma ya majisafi zikiwemo taarifa za mivujo ya maji na ankara za maji za kila mwezi,”alisema Lyaro.

Alisema kuwa kwa sasa wateja hawana haja ya kutumia muda mrefu katika ufuatiliaji wa kuunganishwa huduma ya maji, bali kilichorahisishwa ni mteja kuweka taarifa zake sahihi kwenye mfumo huo na DAWASCO itatumia taarifa hizo kumtafuta mteja na kukamilisha taratibu nyingine hadi kuhakikisha mteja anapata huduma ya maji.
Dawasco kuunganisha maji kieletroniki ndani ya siku 7 Dawasco kuunganisha maji kieletroniki ndani ya siku 7 Reviewed by Zero Degree on 8/08/2017 11:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.