Loading...

Arsene Wenger: Nimealikwa na George Weah kwenye sherehe ya kuapishwa kwake


Meneja wa Arsenal Arsene Wenger ameambia BBC kwamba amepokea mwaliko kutoka kwa rais mteule wa Liberia George Weah kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwake baadaye mwezi huu.

Wenger amesema: "Nimealikwa na George kwa siku hiyo ambapo ataapishwa kuwa Rais."

Meneja huyo wa Arsenal alikuwa meneja wa Weah katika klabu ya Monaco inayocheza Ligi Kuu ya Ufaransa miaka ya 1990 na amesema hakuwahi kufikiria kwamba wakati mmoja mchezaji huyo angekuwa rais.

"Maisha ya jamaa huyu kwa kweli ni kama filamu. Ni ya kushangaza. Yanaweza kuunda filamu nzuri sana," amesema Wenger.

"Nakumbuka nilipomuona mara ya kwanza Monaco alipofika na alikuwa anaonekana kukanganyikiwa kidogo, hakuwa anamjua mtu yeyote, na hakuwa anatazamwa na wengi kama mchezaji stadi na baadaye akaibuka na kuwa mchezaji bora duniani 1995 na leo hii sasa amekuwa rais wan chi. Ni kisa cha kushangaza," Wenger ameongeza.

Wenger alikuwa mkufunzi wa George Weah miaka ya 1990 Monaco
Wenger amesema Weah kwa muda mrefu amekuwa anaipenda sana nchi yake na ana ukakamavu ambao umemfanya kuamini kwamba alikuwa na ndoto fulani maishani.

"Nilisafiri na George wakati huo kulipokuwa na vita nchini Liberia na nimeona jinsi alivyotatizika kutokana na taifa lake na hilo lilikuwa jambo moja ambalo lilikuwa linaendelea kwa muda taifa lake, upendo wake kwa taifa hilo na watu wake," amesema Wenger.

"Leo hii nikitazama nyuma na kumuona akitokwa na machozi vita vilipokuwa vimechacha Liberia ni jambo la kufurahisha sana na natumai atakuwa rais wa furaha na ningependa kuona bwana huyu akiwa mfano mzuri kwa wachezaji wote wa soka wa sasa."

Wenger amesema kwamba hataweza kusafiri Liberia kuhudhuria sherehe hiyo ya kuapishwa kwa Weah kutokana na shughuli nyingi Ligi Kuu ya Uingereza.

"Ninaamini nitakuwa na shughuli nyingi lakini iwapo nitapigwa marufuku basi nitapata muda wa kwenda," Wenger, ambaye amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na Chama cha Soka England amesema.

Weah alishinda duru ya pili ya uchaguzi mwezi jana dhidi ya aliyekuwa makamu wa rais Joseph Boakai kwa kupata zaidi ya 60% ya kura.

Atachukua nafasi ya Ellen Johnson Sirleaf rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuchaguliwa kuongoza taifa la Afrika.
Arsene Wenger: Nimealikwa na George Weah kwenye sherehe ya kuapishwa kwake Arsene Wenger: Nimealikwa na George Weah kwenye sherehe ya kuapishwa kwake Reviewed by Zero Degree on 1/05/2018 05:44:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.