Loading...

Akofu awataka mapadri kuepuka kuwa kituko mitaani


MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo amewaomba waumini wa dini zote nchini, waendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwa mwaminifu katika kutenda kazi ya kumtumikia Mungu.

Pia, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Eusebius Nzigilwa amewataka mapadri kuepuka kuwa kituko mitaani, badala yake wamtumikie Mungu kwa nia moja.

Kardinali Pengo alitoa ombi hilo jana baada ya kuwaongoza mapadri zaidi ya 150 wa jijini Dar es Salaam kurudia kiapo chao cha upadri. Tukio hilo lilifanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph kwenye misa maalumu, inayowakutanisha mapadri na maaskofu kwa pamoja.

Ni misa ya kumbukizi ya siku ambayo Yesu alikutana na mitume na kugeuza mikate kuwa mwili wa Yesu na divai kuwa damu. Pengo alisema njia ya maombi, itamsaidia kuendelea kuifanya kazi ya Mungu vema zaidi, ikiwemo kumtumikia Mungu kikamilifu huku akiwa msafi katika kuitekeleza.

Alisema, anapenda kuendelea kuwatumikia watu kwa nia moja na moyo mmoja kwa muda wote, kwa kuwa ndio kazi ambayo Mungu amleta duniani kuitekeleza.

Kardinali ambaye kwa sasa ana miaka 74, katika misa hiyo alipongezwa kwa kutimiza miaka 20 ya utumishi wa Mungu akiwa kardinali ambapo baada ya misa hiyo alipewa zawadi za pongezi kutokea kwa makundi mbalimbali ya waumini.

Alikaa mbele katikati ya kanisa, huku makundi zaidi ya 20 kupitia wawakilishi wao walimpelekea zawadi mbalimbali, kabla ya waumini nao kupita mbele na kutoa sadaka maalumu kwake, tukio ambalo pia Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda alihudhuria.

Baada ya kupewa zawadi, Askofu Nzigilwa alielezea nia ya Jimbo Kuu Dar es Salaam ya kumjengea nyumba Kardinali Pengo, atakayoishi pindi akistaafu ukardinali. Alisema nyumba hiyo itajengwa Mtoni Kijichi, tofauti na ile ya Kisiju, nje kidogo ya jiji, ambayo alishaanza kujengewa.

Alisema, uongozi wa Jimbo umemuomba Kardinali Pengo, akubali kujengewa nyumba hiyo Kijichi, ili asiende kuishi Kisiju pindi akistaafu. Alisema watamjengea nyumba ya kisasa. Aliwasihi waumini nao kujiandaa ili ujenzi huo utakapoanza, washiriki pia.

“Tunakupongeza kwa kufikisha miaka 20 ya huduma ya ukardinali. Hakika Mungu akuongoze katika kutumikia waumini na watu wote kwa ujumla, sisi kama Jimbo Kuu tumefurahi ulivyokubali kuishi Kijichi na si tena Kisiju, kwa kuwa tutakufikia kiurahisi zaidi,” alisema Askofu Nzigilwa.

Wakati huo huo, Nzigilwa alitoa mwito kwa mapadri hao kuwa wakati wanarudia kiapo chao, waendelee kutenda mema; na si kuishi kama vituko mitaani.

Alisema; Inabidi mumtumikie Mungu daima, kwa moyo wote, mahala popote, mumtumikie kwa mmoja mmoja bila ya aibu, yaani mjiachie kwake wazima wazima na yeye ataendelea kuwasaidia.”
Akofu awataka mapadri kuepuka kuwa kituko mitaani Akofu awataka mapadri kuepuka kuwa kituko mitaani Reviewed by Zero Degree on 3/28/2018 12:15:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.