Loading...

Watanzania zaidi ya milioni 1.5 hatarini kutokuona vizuri


Watanzania takribani milioni 1.7 wana matatizo ya kutokuona vizuri yanayosababishwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho kuona na shinikizo la macho (Glaucoma).

Hayo yamebainishwa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati akizungumza na wahanabari kuhusu maadhimisho ya wiki ya kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa shinikizo la macho.

Dkt. Ndugulile amefafanua kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) watu takribani milioni 7 duniani wana ugonjwa wa shinikizo la jicho kati ya watu milioni 253 wenye matatizo ya kutokuona vizuri, ambao watu milioni 36 hawaoni kabisa.

Ameeleza kuwa, kwa mwaka 2017 jumla ya watu 13,240 walihudhuria kwenye vituo vya afya nchini wakiwa na tatizo la shinikizo la macho, idadi ambayo inakadiriwa kuwa ndogo ikilinganishwa na watu walio kwenye hatari ya kuwa na ugonjwa huo waliopo nchini ambao bado hawajagunduliwa.

“Kwa Afrika ugonjwa wa shinikizo la jicho unachangia asilimia 15 ya watu wasioona, unaathiri watu wenye umri wa miaka 40 na zaidi. Kwa Tanzania inakadiriwa kuwa 4.2% ya watu wenye umri zaidi ya miaka 40 wana ugonjwa huu sawa na watu 440,000, bahati mbaya 70% hadi 90% ya watu hao hawajijui iwapo wana ugonjwa huu,” amesema.

Amesema ugonjwa huo ni moja kati ya magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamau unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo (Neva ya Optiki) ili kuweza kutafsiri kile mtu anachokiona, vile vile unasababisha upofu kwa taratibu sana siku hadi siku bila dalili yoyote katika hatua ya awali.

Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kujitokeza katika vituo vya afya kufanya uchunguzi wa hali ya macho yao kwa kuwa 75% ya visababishi vya kutokuona vizuri vinaweza kuzuilika au kutibika.
Watanzania zaidi ya milioni 1.5 hatarini kutokuona vizuri Watanzania zaidi ya milioni 1.5 hatarini kutokuona vizuri Reviewed by Zero Degree on 3/12/2018 11:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.