Loading...

Wizara yafafanua kuhusu marufuku ya mitumba


WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema sera ya kukuza na kuendeleza viwanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetafsiriwa tofauti na washirika wake na nchi nyingine ikiwemo Marekani.

Kaimu Mkurugenzi wa Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji, Bernard Haule alisema hayo kwa gazeti la HabariLeo Afrika Mashariki. Amesema Jumuiya ya Afrika Mashriki haina nia ya kupiga marufuku mitumba kuingia, bali ina nia ya kuongeza uzalishaji wa ndani wa bidhaa mpya zanguo, viatu na magari ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje nchi.

Haule anasema suala la uendelezaji wa viwanda, hususan vya nguo, bidhaa za ngozi, viatu na magari ni ajenda ya kudumu katika kuendeleza sera ya viwanda kwa nchi wanachama wa EAC. Akijibu swali ikiwa Jumuiya inaendelea na msimamo wake wa kuzuia mitumba kuingia katika nchi wanachama hasa Tanzania, Rwanda na Uganda bila kujali angalizo la Marekani, Haule amesema siyo kweli kuwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeazimia kuzuia mitumba kama wengi wanavyotafsiri.

Anasema ni ukweli usiopingika mitumba ya nguo na viatu bado ni tegemeo kubwa la mavazi kwa wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na hii inatokana na ukweli kuwa viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi katika nchi zote za jumuiya vimezorota au vimekufa. Haule amesema jambo hili halitawezekana Jumuiya hiyo ikikosa sera ya kuboresha na kuimarisha viwanda vya nguo na bidhaa za ngozi.

Amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Februari 20, 2015 ulipitisha azimio la kuimarisha viwanda vya nguo na ngozi na kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji bidhaa hizo na kupunguza utegemezi kwa mavazi ikiwemo mitumba kutoka nje. Katika mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Februari 23, 2018, Wakuu wa Nchi za EAC waliliagiza Baraza la Mawaziri kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza viwanda vya nguo na ngozi ili kufikia lengo la kuwapatia wananchi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bidhaa mpya za nguo na viatu kwa gharama inayoweza kufikiwa na watu wengi.

Anasema lengo hili likifikiwa inawezekana uingizwaji wa mitumba utapungua kwani watu wengi watapata bidhaa mpya. Hata hivyo, hilo likitokea, haliwezi kutafsiriwa kuwa Jumuiya ina lengo la kupiga marufuku mitumba kutoka nje. Jumuiya ya Afrika Mashariki inapata mitumba kutoka sehemu mbalimbali, Marekani na Ulaya.

Mkakati huu wa kukuza uzalishaji viwandani unalenga pia kuzalisha zaidi bidhaa za nguo na viatu kwa kuuza katika soko la AGOA nchini Marekani. Ikiwa Marekani itaelewa lengo la Jumuiya ya Afrika Mashariki siyo kupiga marufuku mitumba bali kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo viwandani, ushirikiano kati ya pande hizi mbili utaimarika na hakutakuwa na athari za kiuchumi na kidiplomasia kama watu wanavyofikiri.
Wizara yafafanua kuhusu marufuku ya mitumba Wizara yafafanua kuhusu marufuku ya mitumba Reviewed by Zero Degree on 3/13/2018 10:24:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.