Loading...

TANROADS yapiga marufuku abiria kushuka basi lifikapo kwenye Mizani


Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tabora Damian Ndabalinze amewataka abiria kutokubali kushuka katika au kusogezwa mbele ya gari pindi wanapofika katika maeneo ya mizani ya kupimia magari.

Alisema kufanya hivyo nao wanakuwa wakishiriki kosa la udanganyifu ambalo ndio linachangia katika uharibifu wa barabara kutokana na uzito uliozidi.

Meneja huyo alitoa kauli hiyo hivi karibuni wilayani Igunga wakati akijibu baadhi ya hoja kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa na Wilaya ya Igunga na wadau wa sekta ya usafiri kujitathimini kwa ajili ya kuja na majibu ya kuondoa ajali za barabarani mkoani humo.

Alisema TANROADS Mkoa wa Tabora haitawavumilia wafanyakazi wa magari ambao watabainika kuwa na tabia ya kuwasogeza mbele au kurudisha nyuma abiria pindi wanapokaribia mizani ili gari lisionekana kuwa limezidisha mzigo.

Ndabalinze aliwaonya pia madereva wa magari madogo madogo kuwa nao watakuwa wanatenda kosa la udanyanyifu ikiwa watashirikiana na madereva wa mabasi makubwa kubeba abiria wao ili kuwavusha katika mizani ili magari hayo yasionekana yamezidisha abiria au mzigo.

Alisema watakaobainika watatozwa faini kali kwa mujibu wa Sheria kwa ajili ya kutoa fundisho kwa wengine ili wasije wakajaribu kufanya udanganyifu ambao ndio unachangia baadhi ya barabara kuharibika mapema.

Alisema udanganyifu mwingine ambao umekuwa ukifanywa na wenye magari kwa kushirikiana na baadhi ya abiria ambao sio wazalendo ni kwa abiria kudai wanakwenda kujisaidia wanapofika katika mzani.

Ndabalinze alisema kuwa ikiwa abiria watashuka kwa ajili ya kwenda kijsaidia gari lisuburi warudi na wakae ndani ndipo utaratibu wa upimaji uendelee.

Aidha alisema ni jukumu la mfanyakazi wa Kitengo cha Mizani kuchungulia katika gari linapofika katika eneo upimaji ili kujiridhisha kama abiria wote wamekaa katika viti.

Meneja huyo wa TANROADS alisema hatamvumilia mtumishi yoyote aliye katika Kitengo cha cha mizani ambaye atabainika kuwa na vitendo vya rushwa na hivyo kushirikiana na wenye magari ili yapite hata kama yamezidisha mizigo.

Aliwataka wasafiri na madereva wakiona vitendo vya rushwa kupiga simu katika namba zilizopo katika vituo vyote vya miazani ili kukoesha tabia hiyo.
TANROADS yapiga marufuku abiria kushuka basi lifikapo kwenye Mizani TANROADS yapiga marufuku abiria kushuka basi lifikapo kwenye Mizani Reviewed by Zero Degree on 4/09/2018 10:06:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.