Loading...

Wabunge waomba kujadili mvua


KUTOKANA na athari zinazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, baadhi ya wabunge wameomba muongozo, wakitaka jambo hilo lijadiliwe kama dharura bungeni, kwa kuwa hali inazidi kuwa mbaya katika maeneo mengi nchini.

Mbunge wa Viti Maalum, Rhoda Konchela (Chadema) amesema bungeni kuwa, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha takriban siku 10, barabara ya kutoka Mpanda-Tabora imefungwa na wakazi wa Katavi wanalazimika kutumia saa 14 kusafiri na wengine kulala njiani.

Amesema baada ya barabara hiyo kufungwa, wananchi hao wamelazimika kutumia njia ndefu ya kuzunguka kupitia Kigoma kwenda Mtwara, jambo linalowaongezea gharama ya usafiri lakini pia kutumia muda mrefu safarini.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) amesema, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, miundombinu katika maeneo mengi imeharibika, kiasi cha baadhi ya mikoa kusitisha baadhi ya huduma na kutoa likizo fupi kwa wanafunzi.

Ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iangalie uwezekano wa kurejesha mfumo wa zamani wa mihula mitatu, badala ya miwili ili kupisha mafuriko, ambayo hujitokeza mwezi wa Aprili na Desemba kutokana na wingi wa mvua.

Alisema kwa sasa hali ya mvua inayoendelea kwenye mikoa, imesababisha mafuriko na maeneo mengi na watoto hawafiki shule kutokana na barabara kutopitika. Mbunge wa Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema) aliomba muongozo Bunge hilo lijadili kama dharura kuhusu athari zinazoendelea kutokana na mvua, kwa kuwa haijulikani zitakatika lini na hali inazidi kuwa tete katika maeneo mengi nchini.

"Mvua zinanyesha sana, hali inazidi kuwa mbaya, wananchi wanataabika kwa mafuriko. Jambo hili linahusu afya. Naomba muongozo, Bunge lako tukufu lijadili suala hili kama dharura ili tutafute namna ya kuwasaidia wananchi," amesema.

Akitoa majibu ya miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema kabla ya mvua hizo kunyesha, wataalamu wa hali ya hewa walishatoa tahadhari kwa lengo la kuhakikisha watu wanachukua tahadhari ili kukwepa athari za mvua hizo.

"Mvua hizi zinanyesha nchi nzima na juzi serikali ilisema maeneo ambayo mawasiliano ya barabara yamekatika Tanroads kwa kushirikiana na Tarura wanaangalia namna ya kurejesha mawasiliano, serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu sana haya matukio ya mvua zinazonyesha nchi nzima," amesema.

Amesema suala hilo haliwezi kujadiliwa kama dharura, kwa kuwa tayari serikali imeshaanza kuchukua hatua za kukabiliana nalo, na lengo ni kuhakikisha maeneo yote yaliyoathiriwa yanarekebishwa na kupitika na hali inarejea kama kawaida.

Akijibu muongozo wa Musukuma, Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha alisema hali ya hewa haitabiriki na itakuwa ni vigumu kubadili mihula kwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Wabunge waomba kujadili mvua Wabunge waomba kujadili mvua Reviewed by Zero Degree on 4/19/2018 06:38:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.