Loading...

Bora kula sumu kuliko fedha za Serikali - Rais Magufuli


RAIS John Magufuli amesisitiza kwamba fedha za Serikali ya Awamu ya Tano hazitaliwa na kuwaonya mkandarasi wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji ambayo wamechukua fedha na kushindwa kukamilisha kazi zao na kutoweka, watakuwa wamekula sumu, tena sumu kali.

Aidha, amesema wafadhili wa nchi mbalimbali zikiwemo za Umoja wa Ulaya (EU), Marekani na Uingereza wanaendelea kutoa ufadhili wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutokana na kuaminiwa katika kusimamia vyema matumizi ya fedha za maendeleo ya wananchi pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi. Rais Magufuli aliyasema hayo jana eneo la Nyandeo, Kata ya Kidatu wilayani Kilombero mkoani Morogoro, wakati wa kuweka jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya Kidatu- Ifakara yenye urefu wa kilometa 66.9 inayojumuisha ujenzi wa daraja la mto Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 130.

Alisema kutokana na kutumia vyema fedha za umma ndiyo maana Serikali ya Tanzania inaaminika na kumedhihirishwa kutokana EU, Shirika la Misaada ya Maendeleo la Uingereza (DIFD/Ukaid) na Shirika la Maendeleo la Kimataifa ya Marakani (USAID), kuwezesha ufadhili wa fedha kiasi cha asilimia 49.15 (Uingereza asilimia 40.13 na Usaid 10.72) katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara. “Nashukuru wafadhili mbalimbali bado wanaipenda Tanzania kwa kusaidia kutoa fedha za maendeleo ikiwemo ya barabara Kidatu- Ifakara,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka makandarasi wa barabara hiyo, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wakala wa Barabara (Tanroads), kuikamilisha kwa wakati na ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa wa Aprili 2, 2020 kwa kuwa tayari fedha zipo za mradi huo, huku akiwataka wananchi wa maeneo hayo waitunze kwa manufaa yao na Taifa. Aidha, aliwaagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi kupitia miradi yote ya maji ili kujua miradi ambayo haijatekelezwa na kutokamilika wakati fedha zimetolewa kwa makandarasi hao warudi kumalizia, kurejesha fedha na wakiwa wametoweka, watafutwe mahali popote walipo ili wakamatwe.

Hivyo aliagiza Takukuru, Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuwatafuta na wafikishwe mahakamani kwa kutumia sheria ya Bodi ya Makandarasi inayotaja kifungo cha miaka minne au mitano jela na kurudisha fedha. Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema ujenzi wa barabara ya Kidatu- Ifakara unafanywa na Kampuni ya Renolds Construction Company Ltd yenye makao yake makuu nchini Nigeria. Profesa Mbarawa alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara unafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi za Ulaya (EDF) ukishirikiana na UKaid na Usaid.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa kujumisha malipo ya fidia, misamaha ya kodi, tozo mbalimbali na uhamishaji wa miundombinu ya umeme na maji na utagharimu kiasi cha Sh bilioni 104.914. Alisema kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha eneo muhimu la Ukuzaji na Uzalishaji wa Kilimo la Ukanda wa Kusini (SAGCOT) na kuwa kiungo muhimu cha barabara kuu ya Tanzam kuanzia Mikumi – Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Londo hadi Lumecha (Songea) na barabara ya kutoka Ifakara – Mahenge.

Alisema barabara hiyo itasaidia kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao na malighafi kutoka na kwenda katika bonde la Mto Kilombero hususani wilaya za Kilosa, Kilombero, Ulanga, Malinyi na maeneo mengine ya Mkoa wa Morogoro na nchi kwa ujumla. Naye Mwakilishi wa DFID nchini, Beth Arthy alisema Serikali ya Uingereza kupitia mashirika yake yataendelea kutoa misaada ya ufadhili wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kutambua umuhimu wake katika kuendeleza ukuaji wa uchumi wa wananchi na Taifa la Tanzania. Naye Balozi wa EU nchini Tanzania, Roeland Van De Geer alisema umoja huo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya nchi mbalimbali yapo tayari kuunga mkono kusaidia maendeleo ya Tanzania.
Bora kula sumu kuliko fedha za Serikali - Rais Magufuli Bora kula sumu kuliko fedha za Serikali - Rais Magufuli Reviewed by Zero Degree on 5/05/2018 07:54:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.