Loading...

Kauli ya Serikali kuhusu ugonjwa hatari wa Ebola


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imetoa tamko kuhusu ugonjwa hatari wa Ebola, ambapo imethibitisha kwamba mpaka sasa ugonjwa huo haupo nchini Tanzania na haujaripotiwa kuwepo, hivyo chombo cha habari kilichochapisha kuhusu ugonjwa huo, kimetakiwa kukanusha taarifa hizo.

Akizungumza na wanahabri jijini Dar es Salaam leo Mei 23, 2018, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile, amesema Serikali imeweka vifaa maalum (scanners) Uwanja wa Ndege wa Dar kwa ajili ya kukagua watu wote wanaoingia nchini iwapo wana viashiria vya maambukizi hayo, na iwapo mtu akibainika anatengwa eneo maalum kili kuchunguzwa zaidi.

Aidha, Serikali imesambaza vifaa vya kinga kwa watoa huduma katika maeneo yanayohofiwa yanaweza kuambukizwa mapema, pia kumetengwa maeneo maalum kwenye mikoa ya mipakani kwa ajili ya kuwaweka watakaodhaniwa kuwa na ugonjwa huo pamoja na kufanya maandalizi ya kitaalam iwapo ugonjwa huo utaingia nchini.

Zaidi, Wizara hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi jinsi ugonjwa huo unavyoambukizwa na njia za kujikinga ili kuepuka kuambukizwa.

Ndugulile amesema dalili za ugonjwa huo huonekana kuanzia siku mbili hadi 21 kuanzia siku ya kuambukizwa ambapo dalili hizo ni homa kali, kulegea mwili, kuumwa kichwa, kutapika, kuhatrisha, vipele, ngozi kuwasha, kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.

Amewataka Watanzania kuepuka kuingiwa au kugusa kitu chochote cha majimaji kutoka kwa mwathirika ikiwemo mate, damu na machozi, pia kuepuka kushughulikia maiti ya mwathirika na badala yake kutoa taarifa kwenye vituo vya afya.
Kauli ya Serikali kuhusu ugonjwa hatari wa Ebola Kauli ya Serikali kuhusu ugonjwa hatari wa Ebola Reviewed by Zero Degree on 5/23/2018 05:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.