Loading...

Yanga, JKU zafungasha virago michuano ya SportsPesa Super Cup


Kichapo cha mabao 3-1 ilichopata Yanga jioni huu kutoka kwa Kakamega Homeboys ya Kenya, kimeilazimisha timu hiyo kurejea nchini baada ya kuondolewa kwenye michuano ya SportsPesa Super Cup inayoendelea nchini Kenya.

Yanga imefungwa mabao hayo katika mchezo wa kwanza wa mashindano hayo ambayo yameanzia hatua ya robo fainali hivyo timu inayofungwa ni lazima iage mashindano na kurudi nyumbani kama ambavyo imekuwa kwa Yanga.

Mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, waliruhusu mabao 2 - 1 katika kipindi cha kwanza, kabla ya kukubali bao la tatu kipindi cha pili na kuwanyima nafasi ya kwenda kucheza na Everton huko England ambapo nafasi hiyo anaipata bingwa wa michuano hiyo.


Yanga sasa imeshindwa kupata ushindi kwenye mechi 11 kati ya 12 ilizocheza hivi karibuni katika mashindano yote ikiwemo Ligi kuu iliyomalizika Mei 28, Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na michuano hii.

Kakamega Homeboys ni timu inayoshiriki ligi kuu ya soka ya Kenya na inashika nafasi ya 9 kwenye msimamo ikiwa imecheza mechi 17, ikishinda 7, sare 3 na kupoteza 7 na ina alama 24.



JKU nayo imeungana na Yanga kuyaaga mashindano ya SportPesa Super Cup kufuatia kupoteza mchezo uliomalizika jioni ya leo kwa kufungwa mabao 3-0 na Gor Mahia FC kwenye Uwanja wa Afraha mjini Nakuru Kenya.

JKU inakuwa timu ya pili kutoka Tanzania kuondoshwa katika michuano baada ya Yanga.

Mabao ya Gor Mahia yamefungwa na Odhiambo, Walusimbi na Meddy ambaye amepigilia msumari wa mwisho na kufanya ubao wa matokeo uwe 3-0.

Yanga na JKU zinatarajiwa kuanza safari ya kurejea nchini kesho na hatimaye Yanga kuanza maandalizi ya kibarua cha Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia FC.

Simba na Singida United ndizo timu pekee zilizosalia hivi sasa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo yanayoendelea huko Kenya.
Yanga, JKU zafungasha virago michuano ya SportsPesa Super Cup Yanga, JKU zafungasha virago michuano ya SportsPesa Super Cup Reviewed by Zero Degree on 6/03/2018 06:55:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.