Loading...

Matumizi sahihi ya Bendera na wimbo wa Taifa

Bendera ya Tanzania.

Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, imewaandikia barua wakuu wa vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na maendeleo ya jamii, vyuo vikuu na vishiriki na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhusu matumizi sahihi ya rangi ya bendera na wimbo wa Taifa.


Barua hiyo iliyoandikwa Novemba 23 mwaka huu ikiwa na kumbukumbu namba CHA-56/193/02/16, inasema wizara hiyo imepokea barua ya maelekezo kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuhusu matumizi sahihi ya bendera na Nembo ya Taifa, na Wimbo wa Taifa.

“Kutokana na makosa hayo Wizara ya Mambo ya Ndani inaelekeza kuwa wimbo wa Taifa utapigwa kwenye dhifa za kitaifa na endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi italazimika kuomba kibali kwa waziri mwenye dhamana,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo imebainisha kuwa, “Wimbo unatakiwa kuimbwa kwa ukamilifu beti zote mbili kwa kuzingatia ‘nota’ na maneno.” Kuhusu rangi za bendera ya Taifa, barua hiyo inasema, “Rangi za bendera ya Taifa ni kijani, dhahabu, nyeusi na bluu. Ni makosa kutumia rangi ya njano na uwiano wa bendera ni 2/3 katika urefu na upana".

Www.eatv.tv, imemtafuta Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo ili kutaka kufahamu endapo mtaala utabadilika katika baadhi ya masomo ambayo yanaeleza kuwa katika bendera ya taifa, rangi ya kijani inawakilisha madini?. Lakini alionekana kushangazwa na kusambaa kwa barua hiyo aliyodai kuwa ni ya kiofisi.

“Unataka ufafanuzi gani? Kwa barua ipi uliyoandikiwa?. Ungekuwa umelengwa wewe ningekupa ufafanuzi lakini sio, walioandikiwa wanaelewa zaidi, sasa sijui unataka ufafanuzi gani?", amehoji Katibu Mkuu huyo.

Dkt. Akwilapo ameongeza kuwa, “Ukiangalia watu walioandikiwa hiyo barua utajua kuwa siyo ya vyombo vya habari, hayo ni mawasiliano ya kiofisi".

Hata hivyo hakutaka kuendelea kutoa ufafanuzi kuhusu barua hiyo inayoonekaa kupiga marufuku kuimbwa kwa Wimbo wa Taifa katika mikusanyiko isiyo rasmi, ikiwemo ya wanafunzi wanapokuwa kwenye gwaride la asubuhi ambako ndiko hupata nafasi ya kujifunza na kukariri wimbo huo.
Matumizi sahihi ya Bendera na wimbo wa Taifa Matumizi sahihi ya Bendera na wimbo wa Taifa Reviewed by Zero Degree on 12/13/2018 11:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.