Aveva, Kaburu wafutiwa mashitaka ya utakatishaji fedha
Dhamana hiyo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.Mil 30, ambapo hatua hiyo inatokana na washitakiwa hao kukutwa na kesi ya kujibu katika mashitaka 7 isipokuwa mawili ya utakatishaji fedha.
Hata hivyo washitakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wamerudishwa mahabusu ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 20, 2019 kwa ajili ya washitakiwa hao kuanza kujitetea akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zachariah Hans Pope.
Kutokana na hatua hiyo washtakiwa hao wamepatiwa masharti ya dhamana kwa sababu mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliwanyima dhamana hayapo.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ambapo amesema jukumu la kuthibitisha shitaka kwa washitakiwa ni ka upande wa mashitaka, pia kwa kosa moja moja na sio kwa kutegemeana.
Hakimu Simba amesema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashitaka ambapo amewakuta na kesi ya kujibu washitakiwa hao katika kosa la 1,2,3,4,7,8 na 9 isipokuwa katika shitaka la 6 na 10 ambayo ni ya utakatishaji fedha.
“Mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliyokuwa yanawanyima dhamana washitakiwa hayapo, je upande wa mashitaka wana pingamizi na dhamana ?,”
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Takukuru, Leornad Swai ameeleza hawana pingamizi ambapo Hakimu Simba aliwapatia masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini 2 watakaosaini bondi ya Sh.Mil 30 kwa kila mmoja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Septemba 20, 2019 kwa ajili ya washitakiwa kuanza kujitetea.
Katika kesi hiyo shtaka la kwanza, linakkabili Aveva na Kaburu ambapo wanadaiwa walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
Katika shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.
Shtaka la tatu linalowakabili Aveva na Kaburu inadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa Dola za 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.
Katika shtaka la nne Aveva katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Kimarekani 300,000.
Shtaka la tano, Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia Dola za Kimarekani 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia Dola za Kimarekani 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.
Shtaka la saba linawakabili Aveva, Kaburu na Hans Poppe ambao wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Kimarekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.
Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.
Shtaka la tisa ni, Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.
Chanzo: GPL
Aveva, Kaburu wafutiwa mashitaka ya utakatishaji fedha
Reviewed by Zero Degree
on
9/20/2019 07:50:00 AM
Rating: