Loading...

Mugabe kuagwa kwa sherehe Jumamosi

RAIS wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe (95).

RAIS wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe (95), anayetarajiwa kuzikwa Jumapili hii (Septemba 14) nchini humo, ataagwa kwa sherehe.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari mbalimbali vya kimataifa, kabla ya maziko, kutatanguliwa na sherehe za kumuaga zitakazofanyika Jumamosi.

Mwili wa kiongozi huyo wa kwanza wa Zimbabwe unatarajiwa kurejeshwa nchini humo kesho kutoka Singapore, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa mpwa wa marehemu Mugabe, familia haijafahamu kiongozi huyo wa zamani atazikwa wapi ingawa wanaamini mazishi yatafanyika katika makaburi ya Mashujaa ya Taifa, kama ilivyopangwa kabla ya kutimuliwa kwake madarakani.

Alisema tangu kuondolewa madarakani shujaa huyo wa zamani wa uhuru mwaka 2017, hali yake ya afya iliendelea kudhoofika.

Katika makaburi hayo ndipo alipozikwa mke wake wa kwanza, Sally Mugabe, eneo ambalo lilijengwa kwa msaada wa Korea Kaskazini.

Sally, alikuwa mmoja wa wanaharakati wa ukombozi wa Zimbabwe, aliyetazamwa na wengi hadi kifo chake kama Mama wa Taifa la Zimbabwe.

Taarifa zinaeleza baadhi ya ndugu zake wanataka azikwe kijijini alikozaliwa cha Kutama, kilichopo katika Jimbo la Magharibi la Mashonaland, kilomita 80 magharibi mwa mji mkuu, Harare.

Ijumaa iliyopita, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangangwa, alimtangaza Mugabe kuwa ni shujaa wa taifa na kutangaza siku za maombolezo kabla ya kuzikwa.
Mugabe kuagwa kwa sherehe Jumamosi Mugabe kuagwa kwa sherehe Jumamosi Reviewed by Zero Degree on 9/10/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.