Loading...

Watumiaji simu wataja kero 10 za vifurushi



Agizo la Serikali kuhusu umalimalizaji kero katika huduma za vifurushi na data katika huduma za mawasiliano limewaibua wa huduma hizo na kutaja kero 10 sugu zinazojirudia, huku wakimwomba waziri aanze nazo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile ametoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) kumaliza kero katika sekta hiyo, zikiwano 10 ambazo watumiaji waliozungumza na Mwananchi wanaamini ndio kubwa.

Miongoni mwa kero hizo ni kulazimishwa kutumia kifurushi usiku, kulazimishwa kucheza kamari, utitiri wa ujumbe wa matangazo, simu za ‘kitochi’ kuunganishwa na data au kuwekewa madeni bila kukopa.

Nyingine ni miamala kutofika kwa wakati kwa wahusika au kurudi, vifurushi vya muda maalumu kupotea muda unapokwisha na mlolongo wa namba za huduma kwa mteja.

Kero hizo zinaibuliwa na baadhi ya waliozungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Mwongozo wa kuwasilisha malalamiko TCRA unamtaka mtumiaji wa huduma hizo kuwasilisha kwanza malalamiko yake kwa kampuni ya simu husika na asiporidhika ayawasilishe TCRA, kisha kamati ya malalamiko ya TCRA na hatimaye katika Baraza la Uamuzi wa Haki.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi walisema hawafahamu utaratibu huo na kuwa wamekuwa wanavumilia kero hizo bila ufumbuzi.

Clementi Safe, mkazi wa Tabata Kisukulu alisema inakera kupokea kifurushi cha muda wa maongezi kwa masharti ya kuzungumza usiku tu, muda ambao watu wanakuwa wamepumzika.

“Ina maana gani kunipa dakika sijui ngapi halafu niongee usiku tu na watu ninaowasiliana nao wamezima simu wamepumzika? Kwa nini kifurushi kisitumike mchana kama sio utapeli nini? Alihoji huku akishauri kuondoa muda wa ukomo wa virufurushi hivyo.

Kitivo Diwani, mkazi wa Shekilango alisema kero nyingine ni mtumiaji wa simu ya ‘kitochi’ kujiunga kifurushi kisha kupatiwa huduma za data angali hatumii intaneti.

“Kwa nini kampuni zisitoe huduma kulingana na aina ya simu anayotumia mteja? Anayetumia kitochi apewe dakika tu lakini kwa sasa naona utapeli tu kuniwekea MB ambazo nazirudisha kwake.”

Lakini Daudi Jonas wa Mbenzi Beach alisema kero nyingine ni huduma mbovu za miamala anazokutana nazo mara kadhaa, akitoa mfano alipotuma pesa zikachelewa zaidi ya saatatu kabla ya kurudishwa kutokana na changamoto za mtandao husika.

Kwa upande wake Samweli Tulo alikutana na kero ya kulazimishwa kuendelea kushiriki kwenye kamari ya kampuni ya simu wakati alishajiondoa.

“Yaani si kwamba nilikosea kujiondoa lakini bado hadi leo nalazimishwa kushiriki na wakati mwingine ninakatwa pesa,” alisema huku akitaja kampuni husika inayofanya hivyo.

Kwa upande wake Yohana Simon ambaye ni mtoa huduma ya miamala ya pesa, vifurushi na data eneo la Sinza madukani, alisema kampuni za simu zimekuwa na uzembe wa kupokea simu (huduma kwa wateja) ili kutatua changamoto za pesa kutumwa katika namba tofauti na hali hiyo hujitokeza mara nyingi. “Matokeo yake mtu aliyepokea pesa anazitoa unabakia mgogoro na mteja, lakini wangekuwa wanapokea haraka inasaidia.”

Mkazi wa Temeke, Jitihada Salmin aliyeamua kuhama laini ya simu anayotumia alidai kuchoshwa na kampuni hiyo aliyotumia kukata dakika zake mara kwa mara na juzi aliweka Sh1,000 aliyotumia kidogo kabla ya kukatwa na hivyo kusajili laini nyingine.

Ezekiel Kweka wa Mbenzi ya Kimara alihoji sababu za kuendelea kupokea meseji za kitapeli za ‘tuma kwa namba hii’ au kupigiwa simu na tapeli anayetukana bila kuona juhudi za TCRA kudhibiti suala hilo.

Kuhusu kero hizo, Mkurugenzi wa TCRA, James Kilaba alinukuliwa na gazeti hili hivi karibuni akikiri uwepo wa kero za vifurushi hivyo na kuahidi kuzishughulikia.

Makampuni ya simu


Meneja uhusiano wa kampuni ya simu ya Airtel, Jackson Mmbando alipotakiwa kueleza ni kwa namna gani wanashughulikia kero hizo aliomba atumiwe maswali lakini hata baada ya kutumiwa hakujibu. Alipotafutwa kwa simu yake haikupokewa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia aliyesema yuko likizo, aliomba pia kutumiwa maswali.

Baada ya kutumiwa aliomba kushirikisha wataalamu kabla ya kujibu lakini hadi gazeti linakwenda mtamboni hakuweza kutoa ufafanuzi huo.

Meneja uhusiano wa kampuni ya Tigo, Wounde Shasael alipotafutwa kwa simu yake licha ya kusema yuko likizo, pia aliomba atumiwe maswali ili kushughulikia ufafanuzi.

Chanzo: Mwananchi
Watumiaji simu wataja kero 10 za vifurushi Watumiaji simu wataja kero 10 za vifurushi Reviewed by Zero Degree on 1/01/2021 11:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.