Loading...

Gamondi: Tunatakiwa kuwa makini, Dodoma Jiji ni wazuri



KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema watakuwa makini katika mchezo wao wa hatua ya 16-bora wa Kombe la CRBD Bank dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwani ni timu iliyowasumbua kwenye mechi ya Ligi Kuu, huku akihofia wachezaji wake kubweteka baada ya kutoka kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha Yanga kimeondoka jana jioni kuelekea Dodoma kwa ajili ya mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye dimba la Jamhuri, jijini humo.

Akizungumza jana, Gamondi alisema wamejipanga vizuri kulingana na mchezo huo kuwa mgumu kwani mashindano hayo ni mtoano na anayefungwa anatoka.

Alisema walipata muda mfupi wa kufanya mazoezi kwa sababu ya kutoka katika mashindano makubwa na anatambua Dodoma Jiji FC mara ya mwisho iliwasumbua.

“Haitakuwa mechi rahisi kwa sababu Dodoma Jiji FC ni wazuri na tuliwahi kucheza nao nyumbani na walitusumbua, mchezo huu tunatakiwa kuwa makini na kucheza kwa tahadhari kubwa ili kufuzu kucheza robo fainali,” alisema Gamondi.

Aliongeza kuwa wanahitaji kutetea mataji yao yote msimu huu na ili kufanikisha malengo yao ni kushinda mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC na kwenda kucheza robo fainali na baadaye nusa na kisha fainali.


Gamondi alisema licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali, lakini anaimani na wachezaji waliopo fiti kwa mchezo huo kwenda kupambana na kupata matokeo mazuri mbele ya wapinzani wao hao.

Yanga itashuka dimbani kesho ikitoka kupoteza kwa mikwaju ya penalti 3-2 dhidi ya Mamelodi Sundowns kwenye mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyopigwa nchi Afrika Kusini Ijumaa iliyopita.

Mechi hiyo ilifikia changamoto ya mikwaju ya penalti baada ya matokeo ya suluhu kwa dakika zote 90 za nyumbani na ugenini.

Chanzo: Nipashe
Gamondi: Tunatakiwa kuwa makini, Dodoma Jiji ni wazuri Gamondi: Tunatakiwa kuwa makini, Dodoma Jiji ni wazuri Reviewed by Zero Degree on 4/09/2024 09:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.