Loading...

Shule 2 zafungwa Dar kupisha mvua



Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jji la Dar es Salaam, shule ya awali na msingi za Tusiime na Fountain Gate wamefunga likizo fupi ya siku mbili kuanzia leo Jumatano, Aprili 24 na 25 2024.

Kwa kutambua Ijumaa ni kumbukizi ya Muungano hivyo wamewakumbusha wazazi masomo yataendelea Jumatatu Aprili 29, 2024.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Aprili 24, 2024, Mmiliki wa Tusiime, Dk Albert Katagira amesema wamefunga shule kwa muda kutokana na mvua zinazoendelea kwa kuwa watoto wamekuwa wakichelewa kufika shuleni na majumbani.

“Tumeona hali imekuwa mbaya watoto wanafika nyumba saa sita usiku kutokana na gari kukaa muda mrefu kwenye foleni kutokana na barabara kutopitika tukaona ni kuwatesa watoto,” amesema Dk Katagira.

Amesema watoto wamekuwa wakiamka mapema lakini wanafika shule saa tatu hadi saa nne asubuhi, hivyo hata utaratibu wa ufundishaji umekuwa ukibadilika.

Dk Katagira amesema kuchelewa kwa watoto kufika shule, kumesababisha kuchelewa kwa vipindi vya asubuhi badala ya kuanza saa mbili wanajikuta wameanza kwa kuchelewa.

Pia, amesema kutokana na kuharibika kwa miundombinu, wamehofia usalama wa watoto wanapokwenda shuleni au kutofika kabisa na sababu hizo zimesababisha wafunge shule kwa siku mbili.

“Wanaokuja na usafiri wa kawaida wanawahi lakini wanaotumia gari la shule wanachelewa kati ya watoto 40 ni watoto 15 wanaweza kuwahi kwa sababu kuna maeneo gari haliwezi kufika kutokana na ukatikaji wa njia na mzazi ameshalipa huwezi kumwambia amlete shule,” amesema.

Rehema Ramadhani, mzazi ambaye watoto wake wanasoma Fountain Gate ya Tabata, amethibitisha ni kweli wametumiwa ujumbe wa kusitishwa kwa masomo kutokana na mvua zinazoendelea.

“Tumetumiwa ujumbe jana kuhusu watoto kutokwenda shule hadi Jumatatu Aprili 29 kutokana na mvua, njia hazipitiki,” amesema Rehema.

Naye Athuman Bilal mkazi wa Tabata Liwiti amesema hajaruhusu mtoto wake kwenda shule kwa kuhofia usalama wa mwanawe kupita kwenye njia zinazojaa maji.

“Sijaona haja ya kulazimisha mtoto kwenda shule kwa kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha mfululizo. Nimemwambia mtoto akae nyumbani maana nakutana na watoto njiani wakiwa wanateseka kwenye mvua,” amesema Bilal.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Shule 2 zafungwa Dar kupisha mvua Shule 2 zafungwa Dar kupisha mvua Reviewed by Zero Degree on 4/24/2024 07:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.