Loading...

Yanga yapeleka malalamiko CAF



Yanga imewasilisha barua ya malalamiko kwa shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) ikituhumu upangaji wa matokeo katika mechi yao dhidi ya Mamelodi Sundowns jana ambapo ilipoteza kwa mikwaju ya penalti 3-2 baada ya dakika 90 za mchezo wa marudiano wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kwa sare tasa jijini Pretoria, Afrika Kusini.

Katika mchezo huo,Yanga ilipata bao katika dakika ya 57 kupitia kwa Stephen Aziz Ki lakini lilikataliwa na mwamuzi Beida Dahane wa Mauritania kwa msaada wa waamuzi waliokuwa katika chumba cha teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi (VAR) wakidai mpira haukuvuka mstari wa goli kwa asilimia 100.

Hata hivyo picha za marudio ya luninga zinaonyesha kuwa mpira huo ulivuka wote mstari wa goli na hivyo bao la Yanga lilipaswa kukubaliwa.

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, uongozi wa Yanga kupitia wakili wake, Patrick Saimon umeandika barua ya malalamiko kwa Caf na kuainisha inachohitaji kifanyiwe kazi.

"Tunaomba uchunguzi wa kina wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kuanika viashiria vyovyote vya kosa la kiutawala na upangaji wa matokeo. Vitendo kama hivi vinaathiri ushindani wa mchezo na vinapaswa kuchukuliwa hatua ili kudumisha uaminifu wa mashindano ya Caf," ilifafanua barua hiyo ya Yanga.
Yanga yapeleka malalamiko CAF Yanga yapeleka malalamiko CAF Reviewed by Zero Degree on 4/06/2024 07:40:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.