Loading...

Migogoro inakimbiza wachezaji wazuri - Azim Dewji

Aliyekuwa mdhamini wa timu hiyo, Azim Dewji.

Kufuatia kuwapo kwa sintofahamu ndani ya Simba, aliyekuwa mdhamini wa timu hiyo, Azim Dewji, ameibuka na kuwataka wanachama na mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi kuacha kunyoosheana 'vidole' na badala yake kutumia muda uliopo kujenga kikosi imara kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Dewji amesema hayo kufuatia viongozi wa klabu hiyo kugawanyika, siku chache baada ya timu yao kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimu wa 2023/2024 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza jijini jana, Dewji, alisema kinachoendelea ndani ya klabu hiyo kwa sasa hakifai na anashauri busara itumike ili kuweka mambo sawa katika kipindi hiki mwafaka cha kuandaa timu kwa ajili ya msimu mpya.

Dewji alisema haipaswi kuwashinikiza viongozi kujiuzulu katika nafasi zao bali kila kiongozi ajiuzulu kwa hiari yake pale anapoona inafaa kufanya hivyo kwa maslahi ya Simba.

"Hatupaswi kutengeneza migogoro, migogoro inakimbiza wachezaji wazuri waliokuwa na mpango wa kujiunga na timu, huu si wakati wa kunyoosheana vidole Wana-Simba, ni muda wa kuijenga timu yetu," alisema Dewji.

Aliongeza kikubwa wanachotakiwa kufanya viongozi ni kuelekeza nguvu katika mchakato wa usajili kwa kuangalia wachezaji wenye viwango na hadhi ya kuichezea timu hiyo.

"Simba tulishatoka katika migogoro, tunapaswa kuangalia wapi tulijikwaa msimu uliopita na kurekebisha mambo kabla ya kuanza msimu mpya, na kama Mo anatoa hela za usajili, anataka kuona pesa zinatumika vizuri na kuleta tija kwenye timu," Dewji alisema.

Naye Makamu wa Rais wa Simba wa zamani, Geofrey Nyange 'Kaburu' amesema anafahamu suala la mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji haujafika mwisho na anashauri wanachama kukutana na kumaliza mchakato huo.

Kaburu alisema kwa sasa suala hii halina nguvu na kinachotakiwa kufanyika ni kuhakikisha wanasajili wachezaji wazuri ambao wataisaidia timu kupata matokeo chanya.

"Kubwa kwa sasa ni kuangalia amani inarudishwa, kuhakikisha usimamizi unakuwa sahihi, ni ukweli mtaani watu wa Simba wanachekwa sana, hii inarudisha nyuma heshima ya mashabiki, lakini inapotokea hali hii, ni wakati wa viongozi kuwajibika ili kuangalia njia sahihi ya kupita," Kaburu alisema.

Taarifa zilizopatikana jijini zinasema Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji 'Mo Dewji' amewataka wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi aliowateua kujiuzulu ili kutoa nafasi ya kuteua wapya ambayo atafanya nao kazi ya kukisuka imara kikosi chao.

Hata hivyo, mapema wiki hii, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka upande wa wanachama wakiongozwa na Issa Masoud, walikaririwa wakidai mwekezaji huyo hajaweka fedha kiasi cha Sh. bilioni 20 kama alivyoahidi.

Masoud alisema Mo Dewji anataka fedha alizokuwa anazitoa kusaidia shughuli mbalimbali za kiutendaji ziwe sehemu ya fedha za uwekezaji.

Mjumbe huyo ameungana na baadhi ya wanachama ambao wanapiga kuhusiana na namna fedha za mwekezaji zitavyotolewa katika kufanikisha shughuli za kila siku za klabu hiyo.

Simba kwa mara nyingine tena, msimu uliomalizika iliishia katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikibeba Ngao ya Hisani na Kombe la Muungano.
Migogoro inakimbiza wachezaji wazuri - Azim Dewji Migogoro inakimbiza wachezaji wazuri - Azim Dewji Reviewed by Zero Degree on 6/13/2024 06:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.