Loading...

Tanzania yatajwa orodha ya nchi zinazokabiliwa na umaskini wa chakula


Tanzania imetajwa ni miongoni mwa nchi 20 ulimwenguni ambazo watoto wake wanakabiliwa na umasikini wa chakula, hivyo kuwa hatarini kupata utapiamlo.

Hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Lishe ya Watoto iliyotolewa mwezi huu na Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF), ikionesha hali ya upatikanaji chakula kwa watoto chini ya miaka mitano.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa asilimia 22 ya watoto nchini wanakabiliwa na umaskini wa chakula kwa kiwango kikubwa na asilimia 59 katika kiwango cha kati, hali inayohatarisha ukuaji wao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 27 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, sawa na watoto milioni 181 wanapata milo isiyozidi miwili kati ya minane inayotambuliwa na shirika hilo.

Kati ya watoto hao, milioni 64 wanaishi Kusini mwa Asia na milioni 54 Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikijumuisha nchi za Tanzania, Uganda, Afrika Kusini, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Misri.

Nchi zingine ni Afghanistan, Bangladesh, China, Côte d’Ivoire, Ethiopia, Ghana, India, Indonesia, Myanmar, Niger, Nigeria, Pakistan, Ufilipino na Yemen.

Miongoni mwa watoto hao, wanne kati ya watano hulishwa tu maziwa ya mama na au bidhaa za maziwa au chakula chenye wanga, kama vile mchele, mahindi au ngano; chini ya asilimia 10 hulishwa matunda na mboga na chini ya asilimia tano hulishwa mayai, nyama, kuku na samaki.

Inaelezwa katika ripoti hiyo kuwa mapato ya kaya si sababu pekee ya watoto kukosa mlo kamili kwa kuwa changamoto hii huwapata watoto walio katika kaya maskini na zisizo maskini.

Ripoti hiyo inatahadharisha kuwa vyakula visivyo na afya na vinywaji vinatumiwa na idadi kubwa, hivyo kuibua wasiwasi wa watoto wanaoishi katika umaskini mkubwa wa chakula.

"Nepal, kwa mfano ina asilimia 42 ya watoto wanaoishi katika umaskini mkubwa wa chakula, hutumia vyakula vyenye sukari, chumvi au mafuta mengi, na asilimia 17 hutumia vinywaji vitamu," inaelezwa katika ripoti hiyo.

Ripoti inataja baadhi ya sababu za wazazi kushindwa kuwapatia watoto wao milo sahihi na inayotambulika kimataifa kuwa ni vita ya Urusi na Ukraine na ugonjwa wa UVIKO -19 na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kukabiliana na utapiamlo wa watoto, UNICEF inashauri serikali na washirika kuwekeza katika hatua za kuboresha upatikanaji milo mbalimbali na yenye lishe kwa watoto na kumaliza umaskini mkubwa wa chakula kwa watoto.
Tanzania yatajwa orodha ya nchi zinazokabiliwa na umaskini wa chakula Tanzania yatajwa orodha ya nchi zinazokabiliwa na umaskini wa chakula Reviewed by Zero Degree on 6/11/2024 01:01:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.