Loading...

TLS tunalo jukumu kubwa sana kuona amri za mahakama zinaheshimiwa - Mwabukusi


Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amesema TLS ina jukumu la kuhakikisha amri za mahakama zinaheshimiwa ili kutotengeneza kizazi kama GEN-Z kilichoko nchini Kenya.

Mwabukusi aliyasema hayo jana baada ya kuapishwa katika mkutano mkuu uliofanyika jana jijini Dodoma, siku moja baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo.

Juzi, mawakili walipiga kura kuchagua Rais mpya na nafasi zingine ndani ya chama hicho na matokeo ya uchaguzi kutangazwa usiku. Hata hivyo, mmoja wa wagombea katika nafasi ya urais, Sweetbert Nkuba, ametangaza kwenda mahakamani kuyapinga kwa madai kuwa kulikuwa na ukiukwaji katika kutangaza matokeo.

Mwabukusi alisema kama amri ambazo zimekuwa zikitolewa na mahakama nchini zitaendelea kutoheshimiwa, basi kuna hatari ya taifa kujenga kizazi ambacho kitakuwa na vurugu na maandamano kama ilivyo Kenya.

“Tukiendelea kukaa kimya vitendo hivi vya watu kupuuza amri za mahakama, wananchi watakosa imani na chombo hiki na kujenga kizazi cha GEN -Z ya Tanzania kama ilivyo sasa kwa majirani zetu Kenya.

“TLS tunalo jukumu kubwa sana kuona amri za mahakama zinaheshimiwa kwani mahakama ni chombo kinacho stahili kuheshimiwa sana, vinginevyo watu wataanza kutembea na mapanga.

“Kwa hiyo ni wajibu wetu kama mawakili kuhahakikisha amri za mahakama zinaheshimiwa, kuna sehemu mahakama ilitoa amri mtu atolewe, lakini hakutolewa sasa hali hii siyo nzuri kabisa kwa taifa,” alisema.

Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, Mwabukusi alisema TLS ina wajibu wa kuhakikisha sheria na kanuni zinazingatiwa ili uwe huru na haki.

“Ni kazi ya TLS ili kupata viongozi wenye sifa na uchaguzi kuwa huru na haki na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika uchaguzi mara kwa mara nchini,” alisema.

Kadhalika, alisema TLS inahitaji kuishirikisha serikali kutambua haki za wananchi wake hasa katika masuala ya umiliki wa ardhi.

“Lazima TLS tuishirikishe serikali kutambua pia, wananchi wanahaki kama inahitaji kuwahamisha eneo fulani, lazima ijue kuwa wao pia, wanayohaki yao ya kumiliki maeneo hayo yenye historia ya maisha yao,” alisema.

Chanzo: Nipashe
TLS tunalo jukumu kubwa sana kuona amri za mahakama zinaheshimiwa - Mwabukusi TLS tunalo jukumu kubwa sana kuona amri za mahakama zinaheshimiwa - Mwabukusi Reviewed by Zero Degree on 8/04/2024 10:40:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.