Wizara ya Nishati yashiriki maonesho ya kimataifa Nanenane Dodoma
📌Taasisi zake zatoa huduma kwa wananchi kwa weledi
📌TGDC yaelimisha wananchi nishati ya Jotoardhi inavyoweza kutumika kwenye mifugo
Wizara ya Nishati ikishirikiana na Taasisi zilizo chini yake inashiriki Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Katika maonesho hayo Wizara inatoa elimu ya utekelezaji wa Sera ya Nishati ya mwaka 2015 na kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi kupitia taasisi zake.
Pamoja na masuala mengine, Wizara pia inatoa elimu mahsusi kuhusu Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Katika Banda la Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wananchi wanafahamishwa kuhusu shughuli za uchimbaji Gesi Asilia na Mafuta, usafirishaji na uchakataji wake, matumizi ya gesi kwenye vyombo vya usafiri wa abiria kama Magari (CNG) na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Aidha, katika Banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wananchi wanajionea moja kwa moja utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kupitia kifaa cha Uhalisia Pepe. Mradi huo kwa sasa umeingiza mashine tatu katika gridi ya Taifa.
Vilevile, wananchi wanapata huduma ya kuunganishiwa umeme kupitia mfumo katika simu janja wa Nikonekt, wanapata elimu ya Nishati Safi ya kupikia kupitia majiko yanayotunza umeme, kushughulikiwa changamoto za mita na kupata elimu ya mabadiliko ya mita za LUKU.
Katika Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wananchi wanapata huduma ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia wadau wa usambazaji na uendelezaji wa teknolojia husika, elimu ya usambazaji umeme vijijini, uendelezaji wa miradi midogo ya umeme na fursa zilizopo katika ujenzi wa Vituo vya Mafuta Vijijini.
Kwa upande wake, Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa juu wa Petroli Tanzania (PURA) inatoa elimu kuhusu shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kueleza mipango iliyopo ya kunadi vitalu vilivyo wazi vya utafutaji wa mafuta na gesi nchini.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) wao wanatoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za udhibiti pamoja na Nishati Safi ya kupikia.
Aidha Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) inatoa elimu kuhusu mipango ya uendelezaji wa nishati hiyo nchini, faida za kutumia Joto ardhi kwa Wafugaji ambalo hutumika kukausha samaki na ngozi za wanyama, kutotolesha vifaranga vya Kuku na Bata.
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kupitia Wataalam wake wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu utaratibu wa kuleta na kupokea mafuta nchini.
Kaulimbiu ya Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nanenane 2024 ni Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Wizara ya Nishati yashiriki maonesho ya kimataifa Nanenane Dodoma
Reviewed by Zero Degree
on
8/03/2024 12:29:00 PM
Rating: