Loading...

Mkuu wa Mkoa wa Iringa aipongeza Tenesco kwa juhudi zake


📍Mkuu wa Mkoa wa Iringa atoa pongezi kwa TANESCO kwa huduma bora na hali thabiti ya umeme

📍MD TANESCO atoa majiko ya umeme kwa kuendeleza kampeni ya nishati safi ya umeme kupikia

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, kwa juhudi za Shirika hilo katika kuboresha huduma ya umeme mkoani humo.

Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya Mkurugenzi huyo Mkoani Iringa Julai 22, 2025 Mhe. James alisema hali ya upatikanaji wa umeme kwa sasa ni ya kuridhisha inayopelekea mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.

“Hali ya upatikanaji wa umeme kwa sasa ni tulivu na ya kuridhisha. Tunatoa pongezi kwa TANESCO kwa huduma bora, ushirikiano mzuri, na utoaji wa taarifa kwa wakati,” alisema Mhe. Kheri James.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, alieleza kuwa lengo la ziara yake ni kukagua maendeleo ya Mradi wa TAZA – mradi wa kimkakati unaolenga kuunganisha Tanzania na Zambia kupitia njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Sumbawanga, ambao hadi sasa ujenzi wa njia ya usafirishaji umefikia asilimia 67 ya utekelezaji. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya takribani trilioni 1.5.

“Nimekuja kukagua maendeleo ya Mradi wa TAZA ambao unaanzia hapa Iringa hadi Sumbawanga. Mradi huu ni wa kimkakati na tunatarajia kuwa njia hii ya kusafirisha umeme itaunganisha Tanzania na Zambia,” alisema MD Twange.

Katika kuendeleza kampeni ya “Umeme ni Nishati Nafuu Zaidi Jikoni”, Bw. Twange alimkabidhi Mkuu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala Bi. Doris Kalasa majiko yanayotumia umeme kidogo, na kusisitiza umuhimu wa kutumia umeme kama nishati safi ya kupikia nyumbani.

“Moja ya ajenda ya TANESCO ni kuhamasisha matumizi ya umeme kama nishati safi ya kupikia. Tunaomba viongozi waendelee kuelimisha wananchi kuhusu faida za majiko haya ili waweze kuyatumia majumbani,” alihimiza.

Mkurugenzi Twange yupo Mkoani Iringa katika ziara ya kikazi ya siku mbili ambayo inahusisha ukaguzi wa miradi mbalimbali ya umeme inayotekelezwa Mkoani humo.







Mkuu wa Mkoa wa Iringa aipongeza Tenesco kwa juhudi zake Mkuu wa Mkoa wa Iringa aipongeza Tenesco kwa juhudi zake Reviewed by Zero Degree on 7/23/2025 08:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.