Loading...

Kesi ya Mbowe na wenzake yaanza kusikilizwa


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imeanza kusikiliza kesi dhidi ya Mbowe na viongozi wenzake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo wanakabiliwa na mashitaka ya kufanya mikusanyiko isiyo halali.

Mahakama hiyo imeyatupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ya kutaka kesi yao ipelekwe Mahakama Kuu ikisema maombi hayo hayana mashiko.

Uamuzi huo ulisomwa mbele ya washtakiwa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John Mnyika.

Wengine ni Mbunge wa Tarime mjini Esther Matiko, Katibu Mkuu wa chama hicho Dk Vicenti Mashinji na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa bunda, Esther Bulaya, hawakuwepo mahakamani ambapo Wakili Peter Kibatala alieleza kuwa walikuwa safarini kutoka Dodoma kuja Dar es Salaam kuhudhuria kesi lakini wakaharibikiwa na gari.

Pia Wakili Kibatala aliiomba mahakama kuipanga kesi hiyo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali Juni 8 ama 15, mwaka huu kwa sababu wao (mawakili) watakuwa katika kesi nyingine Mahakama Kuu.

Baada ya Kibatala, kuwasilisha hoja hiyo, Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi, aliiomba mahakama iwasomee maelezo ya awali washtakiwa hao kesho Mei 16.

Nchimbi alidai kuwa hoja iliyowasilishwa na wakili Kibatala imekuja kwa maneno matupu badala ya maandishi.

Alisema upande wa utetezi wana mawakili zaidi ya wawili na kwamba kutokana na mazingira hayo mawakili waliopo wanaweza kuendelea na kesi na akasisitiza usomaji wa maelezo ya awali uwe kesho asubuhi ama mchana.

Hakimu Mashauri aliiahirisha kesi hadi Mei 16 mwaka huu saa nane mchana ambapo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali PH.
Kesi ya Mbowe na wenzake yaanza kusikilizwa Kesi ya Mbowe na wenzake yaanza kusikilizwa Reviewed by Zero Degree on 5/15/2018 11:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.