Loading...

Afcon 2019: Rais Magufuli aionya Taifa Stars


Rais wa Tanzania John Magufuli leo amekutana na timu ya mpira wa miguu ya taifa hilo inayopambania nafasi ya kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika, Afcon 2019.

Magufuli ameichangia timu hiyo maarufu kama Taifa Stars Sh50 milioni kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Lesotho.

Lakini mchango hou wa Magufuli haukwenda hivi hivi tu bila onyo. "Hizi shilingi milioni 50 nilizozitoa nataka ushindi. Mkifungwa na Lesotho mtazitapika kwa njia nyingine," amesema Magufuli.

Magufuli aliaalika timu hiyo ikulu jijini Dar es Salaam na kula nao chakula cha mchana kama sehemu ya motisha.

"Wanangu nendeni mkashinde, nendeni mkapeperushe vizuri bendera ya Tanzania, lengo letu iwe ni kushinda tu," amesema Mgufuli.

Iwapo Stars watashinda mchezo wao dhidi ya Lesotho mwezi ujao, watakuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa mashindano ya Afcon yatakayofantika mwakani 2019 nchini Cameroon.

Stars inayonolewa na mchezaji nyota wa zamani wa Nigeria Emmanuel Amunike inashika nafasi ya pili katika kundi L wakiwa na alama 5 nyuma ya vinara Uganda wenye alama 10. Cape Verde wapo nafasi ya tatu na alama 4 huku Lesotho wakiburuza mkia na alama 2.

Mara ya kwanza na ya mwisho kwa Tanzania kushiriki mashindano hayo ni mwaka 1980 kipindi ambacho hakuna hata mchezaji mmoja wa sasa alikuwa amezaliwa.

"Tulipata uhuru tukiwa watu Milioni 10 leo tupo watu Milioni 55, aibu kubwa watu Milioni 55 tunashindwa kupata wachezaji 11 wanaoweza kuwaletea Kombe hata la Afrika, hicho huwa kinanisononesha."

Magufuli pia amesema wachezaji hupewa kiburi kwa kupongezwa kwa mafanikio madogo wanayoyapata, "Tunapongezana kwa vikombe vya hovyo hovyo, mara mnaitwa bungeni, mara wapi, wanawapa viburi, lakini kiukweli hatufanyi vizuri," amesema Magufuli.

Naye kaimu nahodha wa Stars, Erasto Nyoni amemuahidi rais Magufuli na Watanzania kwa ujumla kuwa watajituma na kurudi na ushindi dhidi ya Lesotho.

"Tumejisikia faraja kuwa hapa, hatuna maneno mengi sana zaidi ya kukupa shukrani. Hili ni deni kubwa, tutapambana tufanye vizuri mechi ijayo ili tufuzu AFCON,"amesema Nyoni.
Afcon 2019: Rais Magufuli aionya Taifa Stars Afcon 2019: Rais Magufuli aionya Taifa Stars Reviewed by Zero Degree on 10/20/2018 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.