Loading...

Magari 42 ya wizi yanaswa nchini


JESHI la Polisi nchini limeyanasa magari 42 yaliyoibwa katika kipindi cha miezi saba, mengi yakiwa ni aina ya Toyota IST, Spacio, Raum, Carina na Noah.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, alisema jana kuwa magari hayo yamepatikana kutokana na msako mkali uliofanyika hivi karibuni ulioambatana na operesheni ya kupambana na uhalifu wa makosa makubwa, yakiwamo wizi wa magari na silaha.

Alisema operesheni hiyo ilianza tangu Machi hadi Septemba, mwaka huu, na magari hayo yameibwa katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Sirro alisema watuhumiwa 35 wa wizi wa magari walikamatwa katika operesheni hiyo na kwamba magari hayo madogo yameonekana kuibwa kwa wingi zaidi kulinganisha na magari makubwa.

Kutokana na kupatikana kwa magari hayo, aliwaomba wananchi ambao wameibiwa wajitokeze ili kuyatambua.

Pia alisema katika operesheni hiyo, askari walikamata silaha haramu 190, risasi 375 na watuhumiwa 166.

Aidha, alisema kumejitokeza tabia ya baadhi ya Watanzania kukimbilia nchi jirani na kujiunga na makundi ya uhalifu na kufanya matukio ya kihalifu.

Alisema hivi karibuni mkoani Mtwara waliwakamata watuhumiwa 104 wakiwa mbioni kuvuka mpaka wa Tanzania kwenda Msumbiji na walipohojiwa walisema wanakwenda kujiunga na kambi za itikadi kali.

Sirro alisema kutokana na hali hiyo, Jeshi lake linatoa onyo kali kwa wale wote wenye tabia ya kufanya matukio ya aina hiyo kuacha mara moja kwani wakiwakamata hatua kali zitachukuliwa.

Kuhusu usalama wa nchi, Sirro alisema nchi iko shwari licha ya kuwapo kwa matukio machache ya uhalifu ambayo Jeshi la Polisi kwa kushirikina na vyombo vingine vya dola, limeendelea kuyazuia.
Magari 42 ya wizi yanaswa nchini Magari 42 ya wizi yanaswa nchini Reviewed by Zero Degree on 10/20/2018 07:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.