Loading...

Lugola atangaza kiama kwa majambazi


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametangaza neema na wakati huo huo vita kwa Makamanda wa polisi wa mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika kile kinachoonekana vita, Lugola amesema endapo majambazi yatafanikiwa kumuua askari katika tukio lolote, Kamanda wa Polisi mkoa husika ajiandae kutafuta kazi nyingine.

Pia ametangaza kuanzia sasa askari wanaopambana na majambazi na kufanikiwa kuwaua watapandishwa vyeo.

Zaidi amewaahidi makamanda wote wa polisi kuboreshewa stahiki zao na kupewa nyenzo muhimu, lengo likiwa ni kuongeza morali ya kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Lugola alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza alipokutana na kuzungumza na vikosi vyote vya Jeshi la Polisi.

Akizungumza na vikosi hivyo, alisema amelazimika kufanya ziara katika mkoa huo kwa lengo la kuelezea mafanikio ya usalama wa raia na mali zao, lakini pia kutoa pongezi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa, Jonathan Shanna, kwa kazi anayofanya.

Akirejea tukio la hivi karibuni lililotokea mkoani humo la maaskari kufanikiwa kupambana na majambazi mbali na kutoa pongezi, Lugola aliyataka majambazi kujisalimisha yenyewe.

“Nimelazimika kuja Mwanza kutokana na kazi mnayofanya inaonekana wazi tena inaleta faraja kwa Rais wetu Dk. John Magufuli, tambueni mnachokifanya nyinyi polisi ni maelekezo ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema takwimu za Januari 2017 hadi Oktoba 2018, zinaonyesha kuwa Jeshi la Polisi limefanikiwa kupunguza uhalifu kwa asilimia 34.

“Na mimi nasema sitaki kumwangusha Rais wetu, Dk. Magufuli, ndio maana natangaza kuanzia leo ma RPC wote wa Tanzania Bara na Zanzibar nitahakikisha mnapewa stahiki zenu na nyenzo za kufanyia kazi lengo ni kuongeza morali.

“Lakini fanyeni kazi zenu bila woga na msikate tamaa pale changamoto za malalamiko dhidi yenu yanapotokea.

“RPC yeyote Tanzania Bara na Zanzibar kwa sasa ambaye atawahiwa na jambazi na kufanikiwa kuleta madhara kwa askari wetu, atambue huyo hatufai na atafute kazi nyingine ya kufanya, ndio maana nasema hawa askari waliofanya kazi ya kupambana na majambazi katika mapango ya Kishili, naombeni nionane nao tule chakula pamoja lakini lazima wapande vyeo,” alisema.

Lugola pia alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na askari waliopo 45,820 ambao alisema kimsingi hawatoshelezi.

Alisema pamoja na kwamba hitaji halisi la askari ni 92,000, kutokana na hilo aliwaomba kusaidiana na polisi waliopo kuimarisha ulinzi na usalama wao kwa kutoa taarifa mapema za wahalifu.

Lugola pia aliyataka majambazi wote kusalimisha silaha zao na kama wataendelea kuwabipu, Jeshi la Polisi lina salio la kutosha litawapigia muda wowote.

Lugola alisema kama kuna majambazi wana mipango ya kufanya uhalifu ni vema wakasitisha kwani hawatabaki salama.

“Nawatangazia kiama majambazi, tambueni nyinyi ni binadamu sasa mtindo wenu wa kuona mnakaribia kukamatwa mnaanza kurusha risasi zenu za kubipu, hapo mnakaribisha majipu na sisi Jeshi la Polisi tumejipanga.

“Tunafukuzana na muda wa utekelezaji wa ilani ya CCM, hivyo vitendo vya uhalifu viishe, Rais Dk. Magufuli hafurahishwi pale anapoona eneo fulani la nchi halina usalama, mimi kama waziri wa wizara hii ya mambo ya ndani ya nchi sitakubali shughuli za rais zikwame eti sababu ujambazi, naomba mjisalimishe,” alisema.

Awali, Kamanda Shanna, alimweleza Lugola kwamba katika Mkoa wa Mwanza uhalifu umepungua katika nyanja zote huku akibainisha kwamba awali kulikuwa na kesi nyingi za wanafunzi kupewa mimba, wizi wa watoto, magari na ujambazi ambayo yote wamejitahidi kuyapunguza na sasa mkoa upo shwari.
Lugola atangaza kiama kwa majambazi Lugola atangaza kiama kwa majambazi Reviewed by Zero Degree on 11/24/2018 12:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.