Loading...

Bil 2.2/- kupeleka maji kwa wananchi 76,000



WIZARA ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inakarabati Mradi wa Maji wa Ntomoko kwa kutumia Sh bilioni 2.2, ambapo ukikamilika utanufaisha wananchi 76,000.

Akitoa taarifa kuhusu mradi huo, katika kijiji cha Busi, wilayani Kondoa, Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, David Pallangyo amesema mradi huo ulioanza miaka ya 1970 kwa juhudi za Mwalimu Julius Nyerere kwa kuweka kambi ya siku 30 kuchimba mfereji wa kusambaza maji, ulisimama kufanya kazi baada ya muda mfupi kutokana na bwawa lililokuwa likizalisha maji kujaa tope.

Pallangyo alisema wakati huo mradi huo ulilenga kuwapa huduma watu 23, 000 kutoka vijiji 17 vya mradi, lakini sasa idadi ya watu imeongezeka mara tatu, hivyo mradi huo unaokarabatiwa maji yake yatatosheleza vijiji vinne vya Kinkima na Lusangi wilayani Chemba na Makirinya na Kerere Chang'ombe wilayani Kondoa.

"Kutokana na utafiti wa kina uliofanywa, umebaini kwamba chanzo hicho hakitatosheleza vijiji vyote 17 vilivyobaki, wizara ya maji kupitia mamlaka hiyo itafanya utaratibu mwingine kuhakikisha vijiji vinapata maji," alisema.

Ukarabati wa mradi wa Ntomoko kwa miezi 12 utafanyika kwa kuweka mabomba, valvu, zege katika sehemu korofi, pampu itakayoendeshwa na umeme jua, kuweka matangi matatu na marekebisho mengine kukamilisha mradi.

Amesema Duwasa imejipanga kwa kumweka Mhandisi Mkazi wa Duwasa, John Oresti katika eneo la mradi huo, lakini aliomba wahandisi kutoka wilaya za Chemba na Kondoa washirikiane ili kukamilisha mradi katika muda uliopanga.

Akizungumza kabla ya Duwasa na Kampuni ya CRSG ya China kutia saini mkataba wa ukarabati huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo alisema wananchi hao wanatakiwa kuelewa kwamba maji yanahitaji kugharamiwa hivyo wajiandae mradi ukikamilika wajue watalipia maji hayo.

Profesa Kitila alisema ukarabati wa mradi huo ni suluhu la muda mfupi, katika kutafuta suluhu la kudumu la maji kutosheleza vijiji vyote 17, wizara inapanga kujenga bwawa kubwa kwa ajili ya kusambaza maji katika maeneo yote yaliyokuwa yakipitiwa na mradi huo nyakati hizo.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Haja Suli alisema mradi huo wa Ntomoko unategua kitendawili cha shida ya maji ya muda mrefu katika eneo hilo, lakini bado vijiji 17 havitanufaika na mradi huo pamoja na kijiji cha Busi ambacho mradi huo unaanzia.

Kuhusu kijiji na kata ya Busi mahali kilipo chanzo cha maji kutofaidika na mradi wa Ntomoko, Profesa Mkumbo alimtaka mhandisi wa maji Kondoa, Falaura Kifaya kupeleka andiko la kuomba kubadilishiwa bajeti kutoka Sh milioni 36 ilizopewa hadi Sh milioni 300 zinazoweza kusaidia kukamilisha mradi huo.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya China Railway Seventh Group (CRSG) Dong Xianyang itakayokarabati mradi huo, alisema watahakikisha mradi huo unakamilika ndani ya mwaka mmoja kama unavyosema mkataba.

Amesema alishafanya kazi ya ujenzi wa barabara ya Mele-Gonga wilayani Kondoa, hivyo atatumia umaarufu wa kampuni yake ambayo ni miongoni mwa kampuni 500 bora duniani, kuhakikisha anatekeleza mradi huo kwa ufanisi.
Bil 2.2/- kupeleka maji kwa wananchi 76,000 Bil 2.2/- kupeleka maji kwa wananchi 76,000 Reviewed by Zero Degree on 2/13/2019 08:20:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.