Loading...

Kagere aanza kuaga Simba


MBIO za kuwania taji la Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajia kuendelea leo katika viwanja vinne tofauti hapa nchini wakati African Lyon ikiwakaribisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Simba, watakaoshuka Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia saa 10:00 jioni bila ya washambuliaji wao wawili.

Simba yenye kumbukumbu ya kumfunga mtani wake katika mechi iliyopita Uwanja wa Taifa, itawakosa mastraika wake, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere pamoja na beki Juuko Murshid ambao wote wana kadi tatu za njano. 

Kati ya mabao 32, Simba iliyofunga hadi sasa katika mechi 16 ilizocheza, mabao 16 yamefungwa na wachezaji hao wawili huku Kagere akicheka na nyavu mara tisa na Okwi mara saba na kuiwezesha timu yao kuvuna pointi 39 hadi sasa inaposhuka dimbani kucheza na African Lyon iliyohamia Arusha ikiburuza mkia na pointi zake 21.

Aidha, akihojiwa na Redio Ten ya Rwanda 
Kagere alifunguka kuwa baada ya msimu huu ataachana na Simba na kutimkia TP Mazembe ama klabu moja ya Uturuki ambayo hakuwa tayari kuitaja, lakini akieleza timu hizo kuvutiwa na huduma yake.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu aliliambia Nipashe jana kuwa wachezaji wote walioko Arusha wako salama na wanachosubiri ni muda wa mechi ufike.

"Tuko vizuri, naamini tutatimiza malengo yetu yaliyotuleta huku, nyota tutakaowakosa wa kikosi cha kwanza ambao walicheza mechi dhidi ya Yanga ni Okwi, Juuko na Kagere, ila Kagere yeye tuko naye Arusha kwa ajili ya kuendelea kujifua," alisema kwa kifupi meneja huyo.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, aliliambia gazeti hili jana kuwa kikosi chake kimefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya mchezo huo ambao ni muhimu kupata pointi tatu ili kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa.

Aussems alisema wachezaji wote wa timu hiyo wako tayari kwa mchezo huo ambao wanahitaji kuondoka na pointi zote tatu kabla ya kurejea Dar es Salaam kukutana na Azam FC.

"Nimewaambia wachezaji wangu, tuna kazi ngumu ya kufanya na tuna michezo nane ambayo ni viporo mikononi, michezo yote ni muhimu kwetu lazima tupambane, ninaziheshimu timu zote, ninajua ugumu wa wachezaji wangu ni umaliziaji, ninalifanyia kazi hili jambo na inawezekana kuleta mabadiliko kwenye michezo yangu inayofuata, ninachohitaji ni pointi tu," alisema Aussems.

Mechi nyingine za ligi hiyo zinazotarajiwa kuchezwa leo ni kati ya Mwadui FC dhidi ya Biashara United wakati Ruvu Shooting wataikaribisha Kagera Sugar na kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wenyeji Coastal Union wataialika Azam FC.

Ligi hiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika itaendelea tena kesho kwa Mbao FC kuwakaribisha vinara Yanga kwenye Uwanja wa CCM, Kirumba jijini Mwanza na Ndanda FC kuwakabili Singida United kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo mkoani Mtwara.

Chanzo: Nipashe
Kagere aanza kuaga Simba Kagere aanza kuaga Simba Reviewed by Zero Degree on 2/23/2019 03:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.