Loading...

Lissu: Siogopi kurejea Tanzania


Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema haogopi kurejea Tanzania huku akibainisha jinsi kukosa mikutano ya Bunge kunavyomshawishi zaidi kurejea nchini.

Mwanasheria mkuu huyo wa Chadema ambaye alipelekwa Ubelgiji kumalizia matibabu ya majeraha aliyopata mwaka 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi takriban 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake, Area D mjini Dodoma, amesema ana mapenzi makubwa na mijadala ya Bunge lakini kwa bahati mbaya hayuko kwenye mijadala hiyo.

Mbunge huyo anaendelea kuchanja mbuga nchini Marekani katiza ziara zake ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watanzania wanaoishi Marekani jana Februari 11, 2019.

Amesema anajisikia vibaya kuendelea kukosa mijadala ya Bunge kwa vile ni jambo analolipenda mno katika maisha yake.

“Napenda kazi ya Bunge, napenda mijadala ya Bunge. Ninaipenda nchi yangu lakini kwa sasa imekuwa nchi ya kutisha. Nasema nime-miss sana mijadala ya Bunge. Naamini iko siku nitarudi na kuendelea nayo kwa vile napenda sana mijadala,” amesema Lissu.

Lissu amesema hana haja ya kuogopa kurejea Tanzania, akisisitiza kuwa wale wanaomtaka arudi wasubiri hadi atakapoambiwa na madaktari wake kuwa amepona kabisa.

“Kwa hiyo watulie kidogo wasizungumze as if (kama) mtu hataki kurudi. Hakuna mtu aliye-miss Bunge kama mimi na ndiyo maana nawaambia wale wanaotaka nirudi,” amesema Lissu.

“Leo watulie kwanza maana madaktari wangu hawajasema nimepona ila wameeleza ninaweza kunyoosha miguu Ujerumani, Ungereza na hapa Marekani, bado sijapona.”

Amesema ingawa bado naendelea na matibabu Ubelgiji ipo siku ataruhusiwa na kurejea nyumbani.

Amesisitiza yuko tayari kukabiliana na hali yoyote akidai kuwa “sina hiari nyingine mbali ya kuukabili ukweli na kuweka bayana.”

Mwanasiasa huyo ambaye hivi karibuni alielezea ndoto yake ya kuwa tayari kuwania urais mwaka 2020 iwapo chama chake kitaridhia, amesema ataendelea kuzungumza yanayotokea nchini.

“Hata kama nikibaki peke yangu, hata kama wengine wote watakimbia kwa hofu I will stand up and speak up (nitasimama na zungumza),” amesema.

“Mradi nimepona nafikiri nina wajibu kwa dunia na wajibu wangu si kuwaeleza hadithi yangu peke yangu ni kuiambia dunia kuhusu hali ilivyobadilika nchini kwangu.”

Katika mkutano huo mara kwa mara Lissu alilazimika kukatisha kuzungumza kutokana na waliomsikiliza kumpigia makofi.

Kuhusu afya yake hakueleza zaidi mbali ya kusisitiza kuwa madaktari wake bado hawajamueleza lini ataruhusiwa.

Chanzo: Mwananchi
Lissu: Siogopi kurejea Tanzania Lissu: Siogopi kurejea Tanzania Reviewed by Zero Degree on 2/12/2019 03:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.