Loading...

Samia ataja nguvu ya Kiswahili katika mapenzi

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi cheti cha ushindi wa tuzo ya Fasihi, Jacob Julius wakati wa hafla ya utoaji Tuzo ya Kiswahili ya Mabati –Cornell ya Fasihi ya Afrika iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe. Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema lugha ya Kiswahili ina nguvu na nafasi muhimu katika maendeleo ya jamii, siasa na mapenzi.

Samia alisema hayo katika hafla ya utoaji wa tuzo ya Kiswahili ya Mabati- Cornell ya Fasihi ya Kiafrika kwa washindi wa mwaka 2018 iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.

“Tunatumia Kiswahili kwenye siasa, katika kujenga mambo ya kijamii na ndiko tunakoelewa na mambo yanakwenda,’’ alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Viwanda, Joseph Kakunda.

Kiswahili na mapenzi

Samia ambaye katika hotuba yake alijinasibu kama mfuatiliaji mzuri wa machapisho ya kifasihi ikiwamo ushairi, alisema lugha hasa Kiswahili inawaunganisha watu kupitia mapenzi na hatimaye kutengeneza famili na koo.

“Kiswahili kinatuunga kwenye mambo mengi, misemo yake inatufundisha uvumilivu na kujenga familia, ukikizungumza vizuri kwa ulimi ulio laini kama wangu. Nikizungumza maneno ya mapenzi kwa Kiswahili unakuja tu, kwa hiyo kinatujenga kuwa ndugu,” alisema.

Mbali na kuzungumzia mapenzi, Samia katika hotuba yake, alihimiza wadau zikiwamo kampuni za kibiashara kukikuza Kiswahili kwa kuwa kina mchango mkubwa kufanikisha ndoto ya Tanzania ya viwanda.

“Swali muhimu ni kwamba tunawezaje kufikia malengo haya bila lugha....hayo yote hayawezi kufikiwa bila ya kuwekeza vya kutosha katika lugha ya Kiswahili,’’ alisema.

Mtanzania, Mkenya waibuka vinara

Katika tuzo hizo, Zainab Alwi Baharoon wa Tanzania aliibuka mshindi upande wa riwaya na kutuzwa Dola za Marekani 5,000 (Sh 11.45 milioni). Aliandika riwaya isemayo; Mungu Hakopeshwi.

Mshindi upande wa ushairi ni Jacob Ngumbau kutoka Kenya aliyeandika diwani iitwayo ‘Moto wa Kifuu.’ Naye alijinyakulia Dola za Marekani 5,000.

Washindi hao walipatikana kutokana na mchujo wa miswada ya washiriki 116.

Tuzo ya fasihi ya Mabati-Cornell ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na malengo ya kuthamini uandishikwa lugha za Kiafrika, kuhimiza sanaa ya tafsiri baina ya lugha za Kiafrika na kutafsiri maandishi ya lugha nyingine kwa lugha za Kiafrika.

Chanzo: Mwananchi
Samia ataja nguvu ya Kiswahili katika mapenzi Samia ataja nguvu ya Kiswahili katika mapenzi Reviewed by Zero Degree on 2/16/2019 07:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.