Loading...

Dar kuwa moja ya majiji makubwa


JIJI la Dar es Salaam lipo chini ya mpango mkakati utakaoifanya kuwa moja ya majiji matatu makubwa na bora ifi kapo mwaka 2036.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuzinduliwa kwa mpango kabambe wa miaka 20 wa ujenzi wa jiji hilo, unaoweka mikakati mbalimbali ya maendeleo ya eneo la jiji hilo pamoja na yanayolizunguka, ikihusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Mmoja wa waandaaji wake, Dk Camilus Lekule alisema hayo jana wakati akiwasilisha mada kwenye uzinduzi wa mpango huo, ulioanza mwaka 2016 na kuishia mwaka 2036.

Alisema katika kipindi hicho, jiji la Dar es Salaam litaungana na majiji ya Cairo nchini Misri na Lagos nchini Naigeria katika hatua hiyo. Dk Lekule aliitaja miongoni mwa mikakati itakayofanikisha kufikiwa kwa hatua hiyo ni kuendeleza upya maeneo ya makazi holela, baada ya hatua za urasimishaji ili kuboresha makazi na kuinua kiwango cha ujenzi, kitakacholingana na thamani ya ujenzi wa maeneo hayo.

Mikakati mingine ni kuendeleza upya na kuongeza ujazo (densitification) katika maeneo yaliyopangwa ili kuitumia miundombinu iliyopo kwa ufanisi sambamba na kupendekeza vigezo na miongozo bora ya ujenzi. “Pamoja na hayo pia kuanzisha vitovu vipya vya huduma kuu za jiji ili kupunguza msongamano katikati ya jiji, lakini pia kuanzisha mamlaka ya Metropoli ya Dar es Salaam,” aliongeza Dk Lekule.

Aidha alisema mipango mingine kwa jiji hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,800 ni kuhifadhi eneo la katikati ya jiji ili kulinda urithi wa kihistoria na kitamaduni, utakaoenda sambamba na mipango timilifu kwa eneo lote la jiji. Awali, akifungua mkutano wa wadau wa mpango huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema mpango huo umelenga kuondoa changamoto mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam, ambazo kimsingi zimekuwa zikichangia kudorora kwa maendeleo.
Dar kuwa moja ya majiji makubwa Dar kuwa moja ya majiji makubwa Reviewed by Zero Degree on 2/16/2019 07:40:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.