Loading...

Wagombea urais Nigeria waahidi kuyakubali matokeo


Wagombea wawili wakuu wa urais nchini Nigeria wametowa mwito kwa wananchi kutojihusisha na vurugu wakati wa uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa wiki na kutoa ahadi ya kuyakubali matokeo yatakayotangazwa.

Rais Muhammadu Buhari na Atiku Abubakar wameungana na wagombea wengine kusaini rasimu ya makubaliano ya amani mbele ya waangalizi wa kigeni akiwemo kiongozi wa nchi za Jumuiya ya madola Patricia Scotland.

Waliotia saini makubaliano hayo wamewatolea mwito wafuasi wao kujizuia kujihusisha na vitendo vya vurugu au vitendo vyovyote ambavyo huenda vikachangia kuhujumu mitizamo ya kufanyika uchaguzi huru wahaki na wakuaminika nchini Nigeria.

Kadhalika wametoa ahadi ya kuheshimu matokeo ya uchaguzi utakaokuwa huru.

Takriban watu milioni 84 wamejiandikisha kupiga kura siku ya jumamosi katika uchaguzi wa rais na bunge.

Uchaguzi wa magavana wa majimbo pamoja na ule wa mabunge ya majimbo umepangiwa kufanyika mwezi Marchi tarehe 2.

Rais Buhari aliingia madarakani mwaka 2015 kama kiongozi wa kwanza wa upinzani kuwahi kumuondowa madarakani rais aliyekuweko na mpinzani wake wakati huo Goodluck Jonathan aliyekuwa rais alikubali kushindwa.

Kiongozi huyo wa Nigeria amesema uchaguzi wa mwaka huu ni historia nyingine ukiwa unawashirikisha wanawake wengi zaidi na vijana na kuwa na rikodi ya vyama 91 na zaidi ya wagombea 71 wa urais.

Buhari ametoa mwito wa kuwepo ushirikiano mkubwa katika siasa ili kusaidia kuyashughulikia masuala ya yanayoikabili nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Kwa upande mwingine Atiku Abubakar aliyewahi pia kuwa makamu wa rais anayesimama kupitia chama cha Peoples Democratic Party PDP anaitaka tume ya uchaguzi na vikosi vya usalama kutoegemea upande wowote.

Tuhuma kwamba rais Buhari na chama chake cha APC wako mbioni kujiweka tayari kuyabadili matokeo au kufanya wizi wa kura ndio suala kuu linalozitawala kampeini za chama cha PDP wakati pia chama hicho kikiwakumbusha wapiga kura kuhusu uongozi wa Buhari alipokuwa kama mtawala wa kijeshi.

Chanzo: Dw
Wagombea urais Nigeria waahidi kuyakubali matokeo Wagombea urais Nigeria waahidi kuyakubali matokeo Reviewed by Zero Degree on 2/14/2019 07:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.