Loading...

Ajib aacha maswali Yanga


KUFUATIA aina ya ushangiliaji aliouonyesha nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajib, katika mchezo wao dhidi ya KMC baada ya beki, Ally Ally, kuwapatia bao la pili kwa kujifunga, hali hiyo imezua maswali mengi kwa Wanayanga wakijiuliza ni ishara ya kuwaaga au la?

Katika mchezo huo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, ambapo bao la pili lilipatikana kwa beki wa KMC kujifunga kwa kichwa akimalizia krosi safi ya Ajib.

Baada ya bao hilo, Ajib ambaye kwa sasa ni nahodha wa Yanga, alishangilia kwa staili ya kuvua kitambaa chake cha unahodha na kuanza kukipepea juu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Gazeti la Bingwa nyota huyo alisema kwamba, ilikuwa ni furaha iliyopitiliza kuona krosi yake imezaa matunda kwa kupata bao, lakini hakumaanisha chochote.

Alisema mchezaji anapofunga katika mechi au kutoa pasi ya bao, hushangilia kwa namna tofauti inayomjia na hivyo ndivyo ilivyotokea kwake kufanya vile.

“Haikuwa na maana yoyote niliyomaanisha, ila kutokana na furaha ya bao na kuona kazi yangu imezaa matunda nilijikuta nafanya tu vile.

“Hiyo hutokea kwa mchezaji yeyote akifunga au kusababisha ushindi, hushangilia kwa staili tofauti anayoamua mwenyewe,” alisema Ajib.

Ajib ambaye mkataba wake na timu hiyo unaelekea ukingoni, amekuwa akionyesha kiwango kizuri kwa sasa, huku akihusishwa na kuondoka kwenye kikosi cha timu hiyo licha ya yeye mwenyewe kukanusha suala hilo.
Ajib aacha maswali Yanga Ajib aacha maswali Yanga Reviewed by Zero Degree on 3/13/2019 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.