Loading...

Aussems, Miraji watwaa tuzo Ligi Kuu Bara


KOCHA Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Patrick Aussems amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi Septemba huku mshambuliaje wake, Miraji Athumani naye ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora, imeelezwa.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana kuwa Aussems na Miraji wametwaa tuzo hizo baada ya kuwashinda wapinzani wao walioingia nao hatua ya fainali katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na shirikisho hilo.

Ndimbo alisema kuwa kwa mwezi huo uliopita, Simba ilicheza michezo mitatu na kushinda yote, ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Kagera Sugar mabao 3-0 na Biashara United mabao 2-0, ambapo Miraji alikuwa na kiwango kizuri uwanjani kwa mwezi huo na kuchangia kwa asilimia kubwa mafanikio ya timu yake.

Miraji ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Septemba


"Mbali na kucheza katika kiwango cha juu, Miraji alifunga mabao mawili katika mechi hizo tatu na vile vile alitoa pasi za mabao mawili," alisema Ndimbo.

Aliongeza kuwa Miraji alimshinda mchezaji mwenzake kutoka Simba, Meddie Kagere, ambaye pia alitoa mchango mkubwa katika mafanikio ya Simba ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne na Ismail Kada wa Tanzania Prisons.

"Kada naye, kufuatia mapendekezo kutoka kwa makocha wanaohudhuria mechi katika viwanja mbalimbali, ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu, alionyesha kiwango kizuri na kutoa mchango katika michezo ambayo Prisons ilicheza, ikishinda miwili, sare moja, ambapo iliifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, Mtibwa Sugar mabao 3-1 na kutoka sare ya magoli 2-2 dhidi ya Lipuli FC.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Miraji atazawadiwa kikombe na zawadi ya Sh. milioni moja kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, Vodacom pamoja na kisimbusi kutoka Azam TV.

Kwa upande wa Aussems, yeye aliwashinda Mohammed Rishard wa Tanzania Prisons na Abdallah Baresi wa JKT Tanzania, baada ya Mbelgiji huyo kuwaongoza mabingwa watetezi kuweka pointi tisa kibindoni kutokana na mechi tatu walizocheza mfululizo.

Simba ndio vinara wa ligi hiyo baada ya kuwa na pointi 12, wakiwa wamecheza mechi nne wakati watani zao Yanga walioshuka dimbani mara mbili, wana pointi moja na wako katika nafasi ya 19.
Aussems, Miraji watwaa tuzo Ligi Kuu Bara Aussems, Miraji watwaa tuzo Ligi Kuu Bara Reviewed by Zero Degree on 10/05/2019 08:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.