Loading...

Walioomba mikopo elimu ya juu mwisho kesho


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku tatu hadi kesho Oktoba 4, mwaka huu kwa waombaji wa mikopo ambao maombi yao yana kasoro kurekebisha kwa njia ya mtandao.

Ofisa Mawasiliano Mkuu wa HESLB, Veneranda Malima amesema kwa njia ya simu kuwa uamuzi huo unalenga kuwapa fursa wanafunzi hao kuambatisha nyaraka zinazokosekana au kufanya masahihisho katika maombi yao.

“Orodha ya wanafunzi hao na utaratibu wa kufanya marekebisho upo katika tovuti ya HESLB, tunawashauri watembelee tovuti yet una kufanya marekebisho yao kwa njia ya mtandao,” alisema Malima.

Kwa mujibu wa Malima, waombaji pia wanaweza kuingia katika akaunti zao walizotumia kuombea mkopo katika mtandao (olas.heslb.go.tz) na kupata maelezo ya kufanya marekebisho na kusisitiza kuwa wanafunzi hao wanapaswa kutumia siku zilizotolewa kukamilisha marekebisho hayo.

“Orodha hii tuliitoa siku mbili zilizopita ili wajifahamu. Tunategemea watakamilisha ndani ya muda uliotolewa kwani kwa masaa machache tangu tufungua mfumo wa kufanya marekebisho, tayari zaidi ya wanafunzi 460 wameshafanya marekebisho mtandaoni,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Malima, imepokea jumla ya maombi 81,992 kwa mwaka wa masomo 2019/2020, na kati yao, wanafunzi 10,452 waliwasilisha maombi yenye upungufu mbalimbali ikiwemo maombi hayo kutosainiwa, vyeti vya kuzaliwa au vya vifo ambavyo havijathibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

“Mwongozo na elimu tuliyotoa kwa mashuleni, kambi za JKT na kupitia vipindi vya televisheni na runinga kwa miezi mitatu viliwaeleza nyaraka muhimu zinazotakiwa na mambo muhimu ya kuzingatia, lakini kwa bahati mbaya, kuna baadhi bado wamekosea … ni wajibu wetu kuwahudumia na ndiyo maana tunawapa nafasi,” amesema.

Serikali imetenga Sh bilioni 450 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2019/20 unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

Fedha hizo, kwa mujibu wa HESLB zinatarajia kuwanufaisha wanafunzi 128,285, kati yao, wanafunzi 45,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza.

Bajeti kwa mwaka 2018/2019 ilikuwa Sh bilioni 427.5 na iliwanufaisha wanafunzi 123,000.

Chanzo: Habari Leo
Walioomba mikopo elimu ya juu mwisho kesho Walioomba mikopo elimu ya juu mwisho kesho Reviewed by Zero Degree on 10/03/2019 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.