Loading...

Majaketi yenye kamera kudhibiti rushwa kwa trafiki


Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuharakisha mchakato wa matumizi ya majaketi yenye kamera kwa askari wa usalama barabarani, ili kukomesha vitendo vya rushwa ambavyo kwa sehemu, vimekuwa sababu ya ajali.

Dk. Mpango ameyasema hayo jijini Dodoms, alipokuwa akifungua kituo kipya cha polisi cha daraja ‘A’ cha wilaya ya kipolisi Mtumba pamoja na ugawaji wa magari 21.

Amesema wizara hiyo inapaswa kuharakisha mchakato huo wa matumizi ya majaketi ili kusaidia kupunguza rushwa kwa polisi, vitendo ambavyo vimekuwa chanzo cha ajali nyingi nchini.

“Nilikuwa ninazungumza hapa na Waziri (Mhandisi Hamad) Masauni, akanieleza kuwa wako kwenye mchakato wa kuanza matumizi ya majaketi yenye kamera ambayo askari wa usalama barabarani watavaa na yatakuwa yanaonyesha kila kitu na mazungumzo yote yatasikika makao makuu ya trafiki.

“Hivyo basi nikutake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuharakisha mpango huu ili uanze kufanya kazi na kuondoa tatizo la rushwa kwa askari wetu wa kitengo cha usalama barabarani,” amesema Dk. Mpango.

Aidha, amelitaka Jeshi la Polisi nchini kujiimarisha kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwamo matumizi ya kamera za ulinzi (CCTV) ili kudhibiti uhalifu na ajali barabarani.

Pia amelitaka kuongeza matumizi ya roboti pamoja na akili mnemba, lakini pia polisi wapatiwe mafunzo ya mara kwa mara ili kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Amesema kutokana na ongezeko la ajali za barabarani, Jeshi la Polisi linapaswa kupitia upya mfumo wa utoaji wa leseni za udereva pamoja na kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya moto, na kuongeza matumizi ya kamera za usalama.

Waziri Masauni amesema kituo hicho kilichozinduliwa ni moja kati ya vituo ambavyo vimejengwa na serikali ili kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Kituo hichi cha kisasa cha daraja A kimejengwa kwa fedha za serikali, lakini pia magari haya 21 uliyogawa leo yatakwenda kufanya kazi katika Wilaya za Kipolisi nchini, na tumeyagawa katika mikoa ambayo ina migogoro ya wakulima na wafugaji,” amesema Masauni.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura, amesema kituo hicho kimejengwa na wataalam wa ndani kwa kutumia mfumo wa Force Account, kimegharimu Sh. milioni 977 na kitahudumia wakazi wa wilaya nane zinazouzunguka mji wa serikali Mtumba.
Majaketi yenye kamera kudhibiti rushwa kwa trafiki Majaketi yenye kamera kudhibiti rushwa kwa trafiki Reviewed by Zero Degree on 5/13/2024 09:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.