Serikali yasisitiza wadau kuwekeza nishati safi
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme ametoa wito kwa wadau wa mazingira kuwekea mkazo suala la nishati safi ya kupikia katika Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema hapa nchini wanawake hutumia muda mwingi kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato hivyo ni muhimu kupanga mipango ya kushirikisha nishati safi katika masuala ya kijinsia.
Bi. Mndeme amesema hayo leo wakati akifungua Kikao kazi cha Wadau cha Kukusanya Maoni Kuhusu Rasimu ya Mpango Kazi wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya Tabianchi, jijini Dodoma.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimekumba sekta za kiuchumi ambazo wanawake, wanaume, watoto, wazee, vijana na makundi maalum hutegemea kwa maisha yao ya kila siku.
Bi. Mndeme amesema sababu mbalimbali zikiwemo majukumu yao kijinsia, utamaduni, umri, uchumi, mila na desturi huchangia makundi hayo ya jamii kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.
“Hii ni hatua kubwa katika uwezeshaji wa masuala ya jinsia hapa nchini, kama mnavyofahamu, Tanzania ni Mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.
Makubaliano ya Paris yanazitaka Nchi Wanachama kuandaa Mpango Kazi wa utekelezaji wa Programu ya Lima kuhusu masuala ya Jinsia na Mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Serikali yasisitiza wadau kuwekeza nishati safi
Reviewed by Zero Degree
on
7/20/2024 10:29:00 AM
Rating: