Tunatakiwa kuwa bora, ugumu wa wapinzani ni jambo la kawaida - Dabo
Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo aliyepo visiwani Zanzibar na kikosi cha timu hiyo kilichoshuka uwanjani jioni ya jana kuumana na Zimamoto katika pambano la kirafiki, ameanza kunogewa na ubora wa wachezaji wapya wakiendelea kujiandaa na msimu ujao wa mashindano.
Dabo amesema hayo ikiwa ni siku chache tu tangu kuanza maandalizi ya msimu ujao huku ikifahamika kuwa watacheza dhidi ya APR ya Rwanda katika raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kama itavuka hapo itakutana na mshindi kati ya JKU na Pyramids ya Misri.
Msenegal huyo alisema wakati wa mapumziko alikuwa akisubiri kwa hamu kukutana na wachezaji hao ambao hii ni mara yake ya kwanza kufanya nao kazi japo alipata muda wa kuwasoma na kuona ubora wa kila mmoja kabla ya kusajiliwa kwao.
Kilichopo mbele yetu ni kuhakikisha wote tunakuwa katika hali nzuri ya kimwili na kiakili kabla ya kuanza kwa msimu, nimefurahi kuona kila mmoja akiwa na hali nzuri(utimamu), huu ni wakati mzuri kwa wachezaji wapya kuendana na namna yetu ya uchezaji, nimevutiwa na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja," alisema kocha huyo.
Nyota wapya ambao Azam imewasajili katika dirisha hili la usajili ni Yoro Mamadou Diaby kutoka Mali ambaye ametokea katika akademi ya Yeleen Olympique, Frank Tiesse kutoka Ivory Coast alikuwa nahodha wa Stade Malien, Ever Meza ni kiungo kutoka Colombia mwenye uzoefu wa kucheza katika mashindano makubwa ya Copa Sudamericana huko America Kusini.
Wengine ni mshambuliaji kutoka Colombia,Jhonier Blanco ambaye alikuwa mfungaji bora wa ligi daraja la kwanza nchini humo msimu uliopita, wazawa ambao wamesajiliwa ni Nassor Saadun na Adam Adam.
Kuhusu wapinzani wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Dabo alisema; "Jambo muhimu ni kujiandaa, tunatakiwa kuwa bora, ugumu wa wapinzani ni jambo la kawaida katika mashindano kama haya, wala sina presha, naona ni fursa kwetu ya kujipambanua na kupigania beji ya klabu yetu kwenda hatua ya makundi, sisi ni Azam."
Azam inatarajiwa kurudi Dar es Salaam leo Jumamosi ili kujiandaa na safari ya kwenda kambini Morocco kujiandaa na msimu mpya kabla ya kurejea mapema mwezi ujao kuwani mechi za Ngao ya Jamii ikipangwa kuvaana na Coastal Union, huku Simba na Yanga zikimalizana katika mechi nyingine ya nusu fainali.
Tunatakiwa kuwa bora, ugumu wa wapinzani ni jambo la kawaida - Dabo
Reviewed by Zero Degree
on
7/14/2024 01:07:00 PM
Rating: